Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI Mkuu, Kassimu Majaliwa, anatarajia kufanya ziara ya siku nne mkoani
Singida ambapo pamoja na mambo mengine atakagua miradi ya maendeleo na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida,
imeeleza kuwa Waziri Mkuu atanza ziara hiyo kesho Julai 15 hadi Juali 19, mwaka huu ambapo ataanzia katika Wilaya ya Manyoni.
Akiwa katika Kata ya Solya Wilaya ya Manyoni,atapokea taarifa ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Singida ya Solya na kuweka jiwe la msingi na baadaye kupokea taarifa ya mkoa na kisha kuzungumza na watumishi.
Aidha,Waziri Mkuu atapokea taarifa na kutembelea ujenzi wa barabara ya
kilometa 10 Itigi mjini na baadaye kuzungumza na wananchi na jioni ataweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Mtoa na kisha kuzungumza na
wananchi.
Julai 16, Waziri Mkuu, atawasili Wilayani Iramba ambapo atatembelea mradi
wa maji Misigiri,atazungumza na wananchi pamoja na watumishi.
Aidha, Waziri Mkuu, Majaliwa atakuwa katika Wilaya ya Makalama ambako
atatembelea mradi wa ujenzi wa daraja la mawe na baadaye mchana atazindua ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkalama na kusalimiana na wananchi.
Julai 18, atakuwa katika Wilaya ya Ikungi, atapokea taarifa na kutembelea
mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Irisya na mchana atatembelea makazi ya
viongozi wa kitaifa.
Baadaye ataweka jiwe la msingi ujenzi wa Chuo cha VETA na Hospitali ya Wilaya na kuzungumza na wananchi.
Waziri Mkuu atahitimisha ziara yake katika Wilaya ya Singida Julai 19, kwa
kuweka jiwe la msingi ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida na
kuzungumza na wananchi.
Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atatembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ya Mandewa na kuzungumza na watumishi.