*Yasema
Mfuko unatimiza malengo yaliyokusudiwa
*Umeondoa
hofu kwa wafanyakazi na kuongeza kujiamini
*Watwaa Tuzo Maonesho ya Sabasaba 2022.
NA
KHALFAN SAID, SABASABA
SERIKALI
imesema inajivunia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa jinsi umeweza
kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuongeza matumaini kwa Wafanyakazi.
Kauli
hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi
alipotembeela banda la WCF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya
Dar es Salaam yaliyofikia kilele jana Julai 13, 2022.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambao ulianza kutekeleza majukumu yake miaka sita iliyopita, unatoa Fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi kwa mujibu wa mkataba na mwajiri wake.
“Sisi
kama Serikali tunaridhika sana na jinsi mnavyotekeleza majukumu yenu,
mmewaondolea hofu wafanyakazi na sasa wanafanya kazi kwa kujiamini” alisema
Alisema na waajiri nao wamepata fursa ya kujielekeza katika biashara na uzalishaji mali kwani kazi ya kumuhudumia mfanyakazi anapopatwa na madhila yoyote akiwa kazini kama vile kuumia, kuugua na hata kufariki, WCF inachukua jukumu hilo.
“Tunaendelea kushuhudia, pamoja na kulipa fidia Mfuko pia unatoa huduma ya
utengamao na kuwasaidia wale ambao wamepata maumivu kwenye viungo vyao wanapatiwa matibabu na wakati mwingine wanapopona wanarudi kazini na kuendelea na majukumu yao.” Alifafanua.
Wakati
huo huo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeibuka mshindi wa tatu kati ya
Wizara, Wakala na Taasisi zote za Serikali zilizoshiriki kwenye maonesho ya 46
ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (Sabasaba 2022).
Ushindi
huo umetangazwa wakati wa kilele cha Maonesho hayo Julai 13, 2022 ambapo mgeni
rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Philip Isidory Mpango.
Akizungumzia
mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amewashukuru wadau wote
waliotembelea Banda la WCF wakati wa maonesho hayo.
“Tunawashukuru
sana viongozi wa Serikali pamoja na wadau wetu wote waliojitokeza kwa wingi
sana mwaka huu kutembelea Banda la WCF. Kwa pamoja tumeshinda”, amesema
Dkt. Mduma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu (kulia) akipokea majarida na nembo ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kutoka kwa Meneja Mipango WCF, Patrick Ngwila alipotembelea kwenye banda la Mfuko huo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, jana Julai 8, 2022.