Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Rukwa, Dkt. Ismail Macha akikagua moja ya mtambo wa kuzalisha gesi ya Oksijeni katika hospitali hiyo.Muonekano wa jengo la Waagonjwa wa Maututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Mkoani Rukwa.Mwonekano wa Nyumba ya Mtumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga mkoani RukwaJengo la mitambo ya kufua Gesi ya Oksijeni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga mkoani Rukwa.Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Rukwa, Dkt. Ismail Macha (kwanza kushoto) akielezwa na Mhandisi Umeme wa Hospitali hiyo namna mitambo ya kuzalisha gesi ya Oksijeni inavyofanya kazi.Mmoja wa Waajiriwa katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Rukwa, ambaye pia ni mnufaika wa Ufadhili wa Ajira zilizoko chini ya Mradi wa IMF Mhandisi vifaa Tiba Anna Mtega akieleza namna pampu ya kusafirisha hewa ya oksijeni iliyokwisha tengenezwa.
****************
Na. Majid Abdulkarim, RUKWA
Wakazi wa Rukwa wamerahisishiwa upataikanaji wa huduma za afya za rufaa ambazo awali walikua wakizifuata nje ya mkoa kutokana na uboreshaji wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga.
Kauli hiyo imebainishwa leo na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Dkt. Ismail Macha wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma za afya na utekelezaji wa miradi ya afya katika mkoa huo chini ya Ufadhili wa fedha za Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo amesema kuwa zaidi ya Bilioni 3 zimetolewa kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya afya katika Hospitali hiyo.
Dkt. Macha amesema kuwa ufadhili huo umeboresha jengo la wagonjwa wa Dharura, wagonjwa mahututi na Watoto mahututi, jengo la mionzi, jengo la tiba mtandao, nyumba ya mtumishi na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya majengo hayo.
“Kwa upande wa ujenzi wa jengo la Tiba Mtandao, jengo hili limekamilika kwa asilimia 100, jengo la wagonjwa mahututi limefikia asilimia 94, jengo la Radiolojia liko asilimia 85 na nyumba ya mtumishi imefikia zaidi ya asilimia 95”, amesema Dkt. Macha
Akizungumza Dkt. Macha amesema kuwa ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi utaweza kuhudumia wagonjwa 13 kwa wakati mmoja tofauti na awali ambapo lilikuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa sita pekee.
Pamoja na maboresho mengine fedha hizo zimetumika kuajiri wataalamu wa afya katika hospitali hiyo ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kupeleka baadhi ya wataalamu kupata mafunzo ya utoaji huduma kwa wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharura.
Amesema ukarabati wa majengo hayo utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali ambapo wagonjwa walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya Mkoa jirani wa Mbeya.
Aidha,Dkt. Macha ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Afya chini ya Waziri Ummy Mwalimu kwa kuleta miradi hiyo kwa wakati sahihi kwani ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya Uviko 19.