Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dk Angelina Mabula akizungumza na waandishi wa habari leo hii Jijini Mwanza
**********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara ya ardhi inatarajia kukusanya bilioni 250.1 kutokana na maduhuli ya sekta ya ardhi ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ambayo imeanishwa kwenye hotuba ya bajeti.
Hayo yamebainishwa leo hii Jijini Mwanza na Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dk.Angelina Mabula, wakati akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya Wizara hiyo kwa waandishi wa habari.
Vipaumbele hivyo ni kuimarisha matumizi ya tehama,usalama wa miliki za ardhi,kuimarisha miundombinu ya upimaji na ramani,upangaji miji na maendeleo ya makazi,urasimishaji makazi,migogoro ya ardhi,mabaraza ya ardhi na nyumba ya Wilaya, utawala bora na uwajibikaji,tume ya taifa na mipango ya ardhi pamoja na Shirika la nyumba la taifa.
Mabula amesema kuwa Wizara itaendelea kujenga,kusimika na kuimarisha miundombinu wezeshi ya tehama kwa awamu katika ofisi za ardhi za Mikoa na Halmashauri za nchi,sanjari na ukarabati wa mtandao kiambo katika ofisi za Halimashauri 47 zikiwamo makao makuu ya Mikoa ya Iringa,Lindi,Mwanza na Mbeya.
Amesema kupitia mradi wa uboreshaji wa miliki za ardhi (Land Tenure Improvement) ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu,mradi utajenga ofisi za ardhi katika Mikoa 25 zitakazokidhi utoaji huduma kwa mfumo unganishi wa kuhifadhi taarifa za ardhi.
Mabula ameongeza kuwa katika kuimarisha miundombinu ya upimaji na ramani mradi huo utawezesha kuongeza kasi ya upangaji na upimaji ardhi,uwezo wa kuandaa ramani za msingi kwa nchi nzima ambazo zitahitajika kwa matumizi mengine hususani ya ujenzi wa miundombinu na misingi ya umma.
“Katika kulinda maeneo yanayochipuka kuwa miji,Wizara imeandaa mwongozo wa kusimamia uandaaji wa mipango ya uendelezaji wa makazi na ujenzi wa nyumba vijiji ambao unaelekeza namana ya kupanga makazi Vijijini,pia Wizara inaandaa mafunzo kwa Wananchi kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa upangaji na usimamizi kwa miji midogo katika maeneo ya vijijini”,amesema Mabula
Ameongeza kuwa Wizara inatambua umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utawala bora, uwajibikaji ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa sekta ya ardhi,katika mwaka 2022/23 Wizara itaanzisha mfumo wa usimamizi wa sekta ya ardhi (Land Governance Framework) ambao utaongeza uwajibikaji,uwazi na ufanisi katika kutoa huduma za sekta.