Mwakilishi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom anaeshughulikia masuala ya Usimamizi wa Mawasiliano Ester Wangoi akichangia mada wakati wa Kikao-kazi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kilichofanyika Ofisi za TCRA Makao Makuu Barabara ya Sam Nujoma, Dar es salaam. Watoa huduma wamepewa maelekezo ya kuboresha huduma kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano Zenye ubora. Picha na: TCRAMhandisi wa Mawasiliano wa TTCL Sylvester Mbeyale akisisitiza jambo wakati wa kikao-kazi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kilichofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Barabara ya Sam Nujoma, Dar es salaam kujadili namna kampuni za mawasiliano zinavyoweza kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini. Katika kikao hicho TCRA iliwapa maelekezo watoa huduma kuhakikisha wanaboresha huduma katika maeneo yaliyobainishwa kuwa na ubora hafifu. Picha na TCRA
************
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Watoa Huduma za Mawasiliano ya simu nchini wamekutana kujadili mpango wa kuboresha huduma za mawasiliano ya simu hasa katika maeneo ambayo ufikishwaji wa huduma hizo haujafikia viwango stahiki vya ubora. Kikao hicho kilichoketi kwenye Ofisi za Makao Makuu ya TCRA jijini Dar es salaam kiliwakutanisha Vodacom Tanzania, Mic Tanzania (Tigo), Aitel, TTCL, na Halotel na Maafisa wa Idara ya Leseni na Ufuatiliaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
Pande hizo mbili zilijadili namna watoa huduma wanavyoweza kufanyia kazi kwa kurekebisha kasoro za huduma katika maeneo yaliyoainishwa ambapo TCRA mara baada ya kupokea mpango kazi wa watoa huduma itafanya upimaji kwa mara nyingine ili kujiridhisha ikiwa watoa huduma wamefanya maboresho katika maeneo bayana.
Mhandisi Mwandamizi wa TCRA Mwesiga Barongo ambae aliongoza vikao hivyo alibainisha kuwa, pande hizo mbili zimekubaliana masuala kadhaa ambayo yatashuhudia watoa huduma wakitekeleza, kisha kupeleka mrejesho kwa TCRA ikiwa wameboresha huduma.
“Kila mtoa huduma alikuwa na kiwango chake cha matokeo ya upimaji ubora wa huduma; hivyo kwa maeneo yenye upungufu wa ubora tumewaelekeza kwa kuwataka waandae mpango kazi ambao wanapaswa kuutekeleza kwa kuhakikisha maboresho ya huduma kwenye maeneo Kumi na Tano tuliyopima kote nchini, baada ya hapo TCRA tutapima tena kabla mwaka huu kutamatika ili kujiridhisha ikiwa wamefanyia kazi maeneo yaliyobainika kuwa na uduni katika ubora wa huduma” alibainisha Barongo.
Barongo alibainisha baadhi ya maeneo ambayo TCRA iliyapima ili kuthibitisha ubora wa huduma nchini kuwa ni pamoja na Unguja, Pemba, Kyela, Mpanda, Dodoma, Nkasi, Sumbawanga, Moshi, Temeke, Kigamboni, Ubungo, Kinondoni, Ilala, Tabora, na Tanga na kwamba baadhi ya watoa huduma walibainika kuwa na kiwango duni cha utoaji huduma ambapo wamepewa maelekezo kuhakikisha wanapandisha kiwango cha ubora wa huduma.
Katika kikao hicho TCRA iliwaelekeza watoa huduma kuhakikisha wanafanya marekebisho hayo kwa muda mfupi kadri iwezekanavyo na ikiwa watakabiliwa na changamoto hawana budi kuomba usaidizi wa TCRA hasa katika eneo la upitishaji miundombinu ya mawasiliano.
Aidha, watoa huduma walipata fursa ya kutoa ufafanuzi wa namna watakavyoboresha huduma katika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyoainishwa ambayo yalibainika kuwa na changamoto za huduma kupitia chati ya upimaji wa ubora wa huduma ambayo kwenye kikao hicho TCRA kwa pamoja na watoa huduma waliipitia na kukubaliana namna mtoa huduma husika atakavyoboresha huduma.
Wakizungumza pembezoni mwa kikao hicho watoa huduma waliahidi kufanyia kazi maelekezo ya uboreshaji wa huduma.
“Kwa upande wa kampuni yetu tumejidhatiti kuhakikisha tunayafanyia kazi maelekezo yote tuliyopewa na Mamlaka na tutahakikisha tunatekeleza maboresho hayo mapema iwezekanavyo” alifafanua
Mamlaka ya Mawasiliano hufanya upimaji wa ubora wa huduma kwa watoa huduma za mawasiliano kila robo mwaka kisha hutoa taarifa ya upimaji ambayo hulinganishwa na upimaji unaofanywa na watoa huduma ambapo mara baada ya taarifa za pande zote mbili kuletwa pamoja maafikiano ya kitaalamu hufikiwa kisha TCRA hutoa maelekezo kwa watoa huduma kufanya maboresho kwa maeneo ya huduma yaliyobainika kuwa na kasoro