Mbunge wa jimbo la Monduli ,Freddy Lowassa akizungumza katika zoezi hilo la upimaji macho bure wilayani Monduli
Mkurugenzi mtendaji wa Al Ata’a Cheritable foundation ,Ahmed Elhamrawy akizungumza katika hafla huyo wilayani Monduli.
Mratibu wa macho mkoa wa Arusha, Lawrence Mremi akizungumza katika zoezi hilo la upimaji macho bure wilayani Monduli .
**************************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Shirika la Al Ata’a Charitable foundation, linalofadhiliwa na Qatar Charity ya nchini Qatar limetoa msaada wa kupima huduma ya macho bure kwa wananchi kutoka kata mbalimbali za wilaya ya Longido na Monduli mkoani Arusha.
Akizungumza wilayani Monduli Mbunge wa jimbo hilo Fredy Lowassa amesema kuwa ,kitendo cha wafadhili hao kwenda kupima macho kwa jamii hiyo ya wafugaji waishio pembezoni kitasaidia sana kupunguza changamoto hiyo kutokana na uhitaji mkubwa uliopo.
Fredy amesema kuwa,mafanikio hayo yote ya kuja kwa wafadhili hao yamechangiwa na juhudi za Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ya kufungua fursa za utalii kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imechangia maswala mengi kufunguka.
“Tunawashukuru sana wafadhili wetu kwa kuja kutoa huduma hiyo ya macho bure siku tatu na kutoa miwani sambamba na kufanyiwa upasuaji ambapo hadi sasa wagonjwa kumi wameshafanyiwa upasuaji tangu Jana, jambo ambalo linawasaidia Sana wananchi wetu hasa hawa waishio pembezoni kwani wamekuwa wakisahaulika Sana .”amesema.
Aidha amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwani nafasi hizi haziji mara kwa mara, bali zinakuja kwa bahati, hivyo wanatakiwa kujitoa kwani kwa mazoea watu wengi hawana utaratibu wa kwenda hospitali, kwa ajili ya kucheki afya ya macho, ila mpaka mtu apate madhara makubwa kama vile kutoona ndio aende hospitali,” amesema Fredy .
Mkurugenzi Mtendaji wa Al Ata’a Cheritable Foundation, Ahmed Elhamrawy amesema huduma wanayoitoa kwa jamii mbalimbali, ni endelevu ambapo wana programu ambazo wanampango wa kufanya katika sekta ya afya katika magonjwa ya kisukari, moyo na magonjwa ya njia ya upumuaji.
Amesema kuwa, kwa upande wa macho wanakuwa na kambi kwa ajili ya macho, ambapo kwa kila Kambi wanalenga kufikia wananchi 1,000 huku katika hao wakilenga kufanyia upasuaji wananchi 200 kwa kila Kambi ,ambapo amesema mwitikio bado ni mdogo kulingana na matarajio waliyoweka,huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.
Amefafanua kuwa ,wanawafikia watu kulingana na utaratibu wanaopewa na wizara ya Afya juu ya tatizo husika, kwani tatizo la macho ni tatizo kubwa na hasa linahitaji mtu apate matibabu katika hatua za mwanzoni na mtu akichelewa tatizo linazidi kuwa kubwa.
Ameseema kuwa, katika maeneo mengine watu wanashindwa kwenda hospitali kutokana na ukosefu wa huduma hiyo, ndio maana kama taasisi wameenda na vifaa kwa ajili ya kupima na kuwatibu ikiwemo kufanya upasuaji, ili kuwasaidia wanyonge kupata huduma hizo rahisi.
“Mpaka sasa tumeshafanya hizi kambi za macho mara nne katika mikoa mbalimbali hapa Tanzania, ikiwemo mikoa ya Kigoma, Pwani, Dodoma na sasa tupo Arusha katika wilaya mbili za Monduli na Longido” amesema.
Kwa upande wake ,Mratibu wa macho Mkoa wa Arusha, Lawrence Mremi amesema kuwa, wameweza kuwafikia watu 600 katika wilaya ya Longido na zoezi bado linaendelea wilayani Monduli ambapo wilaya hizo zina shida ya wagonjwa wengi wa macho kutokana na eneo lenyewe kuwa kame na upungufu wa maji, pamoja na kuwa na uhaba wa wataalamu wa macho.
Amesema kuwa, changamoto iliyopo ni uhaba wa wataalamu wa macho ambapo kwa halmashauri ya wilaya ya Monduli wapo wataalamu watatu tu katika kitengo cha macho jambo ambalo ni changamoto kubwa hasa katika utoaji wa elimu hasa katika maswala hayo kwani hawatoshi kulingana na idadi ya wananchi wenye uhitaji.
Nao baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hiyo, Naparakwo Laizer kutoka Longido amesema kuwa, jicho lake lilikuwa likiwasha na baada ya kuwa analifikicha mara kwa mara ikifika wakati jicho hilo likawa halioni, lakini amefika katika kituo hicho cha afya na kukuta huduma hiyo ambapo amepata vipimo na baada ya vipimo iligundulika anahitajika kufanyiwa upasuaji wa jicho hilo na baada ya kufanyiwa anaona vizuri.
Naye Mwananchi mwingine Mery Mrina kutoka Monduli amesema kuwa, anawashukuru sana wafadhili hao kwa kuwaletea huduma hiyo hadi nyumbani kwani ameweza kupimwa macho na kupewa miwani bure,huku akiwataka kuwatembelea mara kwa mara na kwenda maeneo ya vijijini kulipo na wahitaji wengi zaidi na hawana sehemu ya kupata huduma hiyo.