*************************
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI Julai 13, 2022 amefungua mafunzo ya siku tatu kwa maafisa wasimamizi na watekelezaji wa sheria ya kuzuia na kupambana na Usafirishaji haramu wa binadamu yanayofanyika katika ukumbi wa BEACO Jijini Mbeya.
Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la TANZANIA RELIEF INITIATIVES ambalo nalo linafadhiliwa na Taasisi ya Hans Saidel Foundation lenye makao yake Makuu nchini Ujerumani.
Akiwa mgeni rasmi Kamanda Matei amelipongeza shirika hilo kwa kuchagua mkoa wa Mbeya kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo na kuwataka maafisa kutoka Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji, Idara ya Mahakama na Ustawi wa Jamii kutumia mafunzo hayo kuleta chachu katika kuzuia na kupambana na Usafirishaji haramu wa binadamu.
Pia ameitaka jamii kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kuhakikisha wanatoa taarifa ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
“Tatizo hili linaweza kuonekana ni dogo hapa nchini lakini ukweli ni kwamba sote tunafahamu kuwa ni kubwa na limeendelea kukua kila mwaka” amesema Kamanda Matei.
Takwimu zinaonyesha kuwa wahanga wanaokolewa katika uhalifu wa Usafirishaji haramu wa binadamu wengi wanatoka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Kigoma, Geita, Dodoma, Mbeya, Iringa, Singida, Arusha, Manyara Shinyanga, Simiyu, Lindi, Mtwara na Zanzibar.
Usafirishaji wa ndani ya nchi ni mkubwa zaidi ukilinganishwa na idadi ya Watanzania wanaosafirishwa kiharamu kwenda nje ya nchi.
Aidha Kamanda Matei amezitaka idara zote za serikali na zisizo za serikali, jamii kwa ujumla kuungana pamoja katika kuzuia na kupambana na Usafirishaji haramu wa binadamu kwani Mbeya ni miongoni mwa waathirika wa matukio hayo.