Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dk,Angelina Mabula akizungumza na viongozi wa dini
Viongozi wa dini mbalimbali wakiwa kwenye mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 na mapambano dhidi ya ukatili.
Katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela Said Kitinga Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye mafunzo ya kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 na mapambano dhidi ya ukatili kwa viongozi wa dini
……………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Viongozi wa dini wametakiwa kuendelea kusaidia katika suala la malezi ya kiroho ili kuweza kujenga jamii yenye kumcha Mungu na uadilifu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dk,Angelina Mabula wakati wa mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 na mapambano dhidi ya ukatili kwa viongozi wa dini mbalimbali waliopo katika Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza.
Amesema viongozi wa dini wana idadi kubwa ya waumimini hivyo watumie fursa hiyo kuwafundisha upendo ili waweze kuwa na hofu ya Mungu hali itakayosaidia kuondokana na vitendo vya kikatili.
Mabula ameongeza kuwa viongozi wa dini wanapokuwa kwenye nyumba zao za ibada wawaelimishe waumini wao ili waweze kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.
Ameongeza kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio yanayohusisha mauaji ya raia kwa raia na baadhi ya watu kujinyonga ambapo amesema tayari Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulitaka jeshi la polisi kuweka mikakati ya kuhakikisha Jamii inatoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vya kihalifu.
Kwa upande wake mratibu wa sensa Mkoa wa Mwanza Goodluck Lyimo, amesema zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa kuwa linaipatia Serikali takwimu za msingi zinazotumika kutunga sera,kupanga mipango pamoja na kuleta maendeleo kulingana na idadi ya watu husika waliopo Nchini.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli lilipo Jijini Mwanza Jacob Mutashi, amesema kuwa ili kuweza kudhibiti vitendo vya ukatili kwa wanandoa na familia kwa ujumla ipo haja kubwa ya viongozi wa dini kufanya vikao mara kwa mara na wanandoa hao kabla na baada ya kufunga ndoa.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto (KIVULINI) Yasin Ally ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwaelimisha waumimini wao kuwalea Watoto katika maadili mazuri ili kuweza kuwaepusha na vitendo mbalimbali vya ukatili vikiwamo mimba za utotoni, ulawiti,uvutaji wa bangi pamoja na utoro mashuleni.
Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Katibu tawala wa Wilaya hiyo Said Kitinga amesema hakuna Nchi ambayo ilifanikiwa kuyafikia maendeleo bila kuwa na takwimu sahihi hivyo amewataka viongozi wa dini kufikisha elimu waliyoipata kwa Wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.