*********************
Na Selemani Msuya
UTELELEZAJI wa Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG), katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania utachochea ukuaji wa uchumi, maendeleo na huduma za kijamii kwa wananchi na mikoa hiyo.
Mradi huo ambao uwekezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka 2025 mkoani Lindi na kukamilika 2030 unagharimu Sh.trilioni 70.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), lililopo Viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba Temeke jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya PURA Halfani Halfani alisema mradi wa LNG unaenda kufanya mapinduzi kwa wananchi mikoa ya Kusini ambayo ni Lindi, Mtwara na Pwani.
Halfani alisema mradi wa LNG ukitekelezwa kwa kiwango ambacho kinarajiwa gesi nyingi itazalishwa na kutumika nchini na nyingine kuuzwa nje hivyo kuongeza ajira.
“Katika utelelezaji wa mradi huu ajira zisizo za kudumu zaidi ya 10,000 zitapatikana.Mfano wauza nondo, saruji, kokoto, vyakula na vingine, hivyo mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa na mapinduzi ya kiuchumi na jamii yataonekana,”alisema.
Halfani alisema PURA itaendelea kutafuta wawekezaji ambao watawekeza katika eneo la mafuta na gesi ambalo limeonesha mafanikio makubwa katika kuinua uchumi wa nchi nyingi.
Alisema pia PURA inaendelea kuunganisha kampuni za Kitanzania ambazo zinazotaka kushiriki utafutaji na uchimbaji gesi na mafuta kupata nafasi.
Mwenyekiti alisema uamuazi wa Serikali kuruhusu uchimbaji wa gesi asilia umewezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwa na uhakika wa nishati ya umeme na ambao unatumiwa na wananchi wengi mjini na vijijini.
Alisema pia wanahamasisha wananchi kutumia gesi asilia majumbani kwa kuwa ni salama kwa wananchi.
“Mimi nasisitiza majadiliano yaendelee kuwa mazuri, ili lengo la Serikali kuzalisha gesi asilia ya LNG yafanikiwe kama yalivyopangwa,” alisema.
Aidha alisema PURA imekuwa ikishawishi Watanzania kushiriki kwenye miradi mbalimbali ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi ambao mwitikio umeanza kuonekana.
Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni wa Kampuni ya Solution Tag Consultant Limited, Tumain Abdallah alisema PURA imekuwa kiungo muhimu wa wao kupata kazi kwenye miradi ya uchakataji gesi asilia.
Abdallah alisema kwa muda mrefu kampuni za wazawa zilikuwa haziaminiki ila kupitia PURA wameaminika na kupewa kazi za ushauri wa masuala ya mafuta na gesi.
“PURA imewaaminisha wawekezaji kuwa sisi tunaweza na hatujawaangusha, kwani tunaendelea kutoa huduma za masuala ya gesi na mafuta kwa kiwango kikubwa,”alisema.
Alisema kampuni yao ina wafanyakazi wazawa tisa ambapo ameshauri vijana Wakitanzania ambao wamesoma mambo ya gesi na mafuta kujitokeza kushiriki.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Uchimbaji Gesi na Mafuta (OGAWOGA), Frank Mwankefu alisema ujio wa PURA umeweza kuwafanya watambulike na kupata kazi katika miradi ya Songo Songo na kwingine.
“Hii PURA imetufanyia mambo makubwa sisi wachimbaji wa mafuta na gesi, tunaahidi kutowaangusha,” alisema.