*************
Na.WAF,Kilimanjaro
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ameutaka Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Mawenzi Mkoani Kilimanjaro kujitazama upya katika usimamizi na uwajibikaji wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa hospitalini hapo.
Prof. Makubi ametoa kauli hiyo leo tarehe 10 Julai, 2022 wakati akikagua ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika jengo la kuwahudumia wagonjwa wa dharura (EMD), wagonjwa mahututi (ICU) pamoja na ujenzi wa jengo la Uzazi, Mama na Mtoto.
Prof. Makubi ameuagiza Uongozi huo kukamilika kwa mradi wa Jengo la mama na mtoto katika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
Pro. Makubi amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo litasaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga na hivyo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona mama mjamzito anajifungua salama na vifo vya watoto wachanga vinapungua,hivyo ubora wa huduma ndio msingi wa sekta yetu ya afya”.Amesema Prof. Makubi
Aidha, ameutaka uongozi wa Hospitali, wakandarasi-MCB na TAMESA kuunganisha nguvu zao kwa pamoja ili kuhakikisha ukamlishaji wa ujenzi hauchelewi tena.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa hospitali hiyo imeanza kupokea vifaa na wameanza kuvitumia kwa jengo la wagonjwa wa dharura(EMD) pamoja lile la wagonjwa mahututi (ICU)
Ameongeza kuwa kukamilika kwa ukarabati wa jengo la Wagonjwa mahututi(ICU) litaweza kuwahudumia wagonjwa mahututi wapatao 16 kwa mpigo ambapo vitanda 16 vimewekwa katika jengo hilo.