NA MWANDISHI WETU, SABASABA
SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya kazi kubwa kuhakikisha Mfuko wa
Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unaweza kulipa mafao stahiki na endelevu, Waziri
Mkuu (Mstaafu) Mhe. Mizengo Pinda amesema.
Mhe.
Pinda ameyasema hayo wakati alipotembelea banda la WCF kwenye Maonesho ya 46 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere
(Maarufu Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
“Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha
Mfuko huu ili kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili waajiri hususan wa
Sekta Binafsi ambao walilazimika kupoteza muda mwingi wakati wafanyakazi wao
walipopatwa madhila yaliyotokana na kazi.” Alisema.
Mhe.
Pinda ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuchangamkia fursa kwa kujiunga na kuwachangia
wafanyakazi wao WCF ili kulinda biashara zao na wafanyakazi wao.
Amesema,
kuna kazi kubwa ya kuelimisha waajiri na wafanyakazi nchini ili kufahamu kwa
ufasaha nini wanaweza kupata kutoka WCF.
Amepoungeza
Mfuko huo kwa kuweka misingi imara na madhubuti iliyowezesha Shirika la Kazi
Duniani ILO kuthibitisha uwezo wa Mfuko huu katika ulipaji wa fidia stahiki na
endelevu kwa wanufaika wake kwa zaidi ya miaka 30 ijayo.
“Nimefurahishwa na tathmini ya ILO
kuhusu uhai wa WCF na ulipaji wa fidia ikiwemo malipo ya pensheni kwa
wafanyakazi waliopata ulemavu wa zaidi ya asilimia thelathini (30) na wenza wa
wafanyakazi waliofariki kutokana na kazi. Hili ndio lengo haswa la kuanzishwa
kwa Mfuko huu na Serikali inajivunia sana kuona matunda ya kuanzishwa kwake”
alisisitiza, Mhe. Pinda.
Alisema
kuwa malipo ya fidia kwa wafanyakazi yanaleta hamasa kwa waajiri wote nchini
pamoja na wawekezaji kwani kwa kufanya hivyo, Tanzania inakuwa kituo sahihi cha
biashara na uwekezaji.
Naye
Naibu Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb),
amewahimiza waajiri wote nchini kuchangia WCF ili wafanyakazi wao wanufaike na
huduma zinazotolewa na Mfuko endapo wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na
kazi.
“Jitahidini
mjiunge na WCF na muione hii kama fursa kwenu na sio mzigo kwa sababu itawapunguzia
malalamiko yasiyo ya msingi endapo wafanyakazi watapata ajali, ugonjwa au kifo
kutokana na kazi,” amesisitiza Mhe. Kikwete.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema WCF itaendelea kufidia wafanyakazi
waliopata ulemavu kutokana na kazi pamoja na wategemezi wa wafanyakazi
waliofariki kutokana na kazi.
Waziri Mkuu (Mstaafu) Mhe. Mizengo Pinda (Kushoto), akisalimiana na Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete walipokutana kwenye banda la Mfuko w aFidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Mhe. Pinda na Maafisa wa WCF wakishuhudia wakati Mhe. Kikwete anatia saini kitabu cha wageni
Mhe. Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Mwanasheria mwandamizi wa WCF, Bw. Deogratius Ngoi
Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na Afisa Tathmini za madai, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Matilda Rusibamayila.