************************
Na Mwandishi Maalumu
OFISI ya Msajili wa Hazina (OMH) imefanikiwa kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh bilioni 852.98 ikiwa ni asilimia 109.50 ya lengo katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22 ulioishia Juni 30, mwaka huu.
Awali, ofisi hiyo inayosimamia Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali na Kampuni ambazo Serikali ina hisa, katika mwaka huo ilipangiwa kukusanya Sh bilioni 779.03.
Kwa mujibu wa Taarifa kwa Umma ya Ofisi ya Msajili wa Hazina iliyosainiwa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto, kiasi kilichokusanywa ni ongezeko la Sh bilioni 214.11 kutoka Sh bilioni 638.87 zilizokusanywa mwaka 2020/21 ikiwa ni sawa na ukuaji wa asilimia 33.50.
Benedicto katika taarifa hiyo amesema ongezeko hilo ni matokeo ya kuimarika kwa shughuli mbalimbali za uchumi chini ya uongozi madhubuti wa Rais Samia Suluhu Hassan ambao umechochea uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.
Alisema sababu nyingine ni uhusiano mzuri kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi zote inazozisimamia; kudhibiti matumizi pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inayosimamia taasisi, mashirika ya umma, wakala za serikali na kampuni ambazo Serikali ina hisa pamoja na kupongeza kwa upatikanaji wa fedha hizo zinazokwenda kufanyakazi kuleta maendeleo ya nchi kwa kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali na hatimaye ukuaji wa uchumi wa Taifa, wameendelea kukumbusha uzingativu wa dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”.
Aidha, imetaka kuzingatiwa kwa dhima kuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2022/23 ambayo ni “Kuongeza Kasi ya Kufufua Uchumi na Kuimarisha Sekta za Uzalishaji kwa ajili ya Kuboresha Maisha”.
“Ofisi ina matumaini makubwa kwa Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali na Kampuni ambazo Serikali ina hisa katika kuboresha utoaji huduma, kukuza biashara na kuhakikisha kuna tija kwenye utekelezaji wa shughuli zao zote,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Benedicto.
Alisema ofisi yake itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu uwekezaji wa serikali kwenye taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina hisa pamoja na kuishauri serikali kuhusu uwekezaji kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za serikali.
Alitaka menejimenti zote kutambua kuwa “Uwekezaji ni Msingi wa Maendeleo Endelevu” na kuendelea kuchagiza maendeleo kwa fikra hizo.
Ofisi ya Msajili wa Hazina ndiyo msimamizi mkuu wa uwekezaji wa Serikali kwa niaba ya Rais na imekuwa pia na jukumu la kusimamia Ubinafsishaji wa Mali za Umma, Usimamizi na Ufuatiliaji wa Mashirika ya Umma, Ukusanyaji wa Madeni ya Serikali yaliyorithiwa kutoka kwa lililokuwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), na Urekebishaji na Ufilisi wa Mali zisizozalisha faida katika kampuni au mashirika yaliyobinafsishwa.
Kwa sasa, Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia Taasisi na Mashirika ya Umma 287, ikijumuisha kampuni na Taasisi 40 zinazomilikiwa na Serikali kwa hisa chache na Taasisi 10 za nje ya nchi 10.