************
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amevitaka vilabu vya michezo kufanya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ili kuinua michezo.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli leo Julai 7, 2022 kwenye usiku wa utoaji wa Tuzo za Mashindano ya NBC ya Shirikisho la soka nchini 2022.
Ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu na watendaji wa sekta ya michezo.
Katika tukio hili lililovuta hisia za wanamichezo ndani na nje ya nchi tuzo 43 katika maeneo mbalimbali zinatolewa huku tukio hilo likirushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam na mitandao mbalimbali ya kijamii kutokea jijini Dar es Salaam.
Mhe amesisitiza kuwa wakati umefika wa Vilabu vya Tanzania kumiliki viwanja vyao kama vilabu vingine duniani ambapo ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa(BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kuratibu kikao baina yake na viongozi wa vilabu mapema juma lijalo ili kujadili utekelezaji wa suala hilo.
“Ninaagiza BMT na TFF wiki ijayo ratibuni kikao na viongozi wa vilabu tulimalize suala hili.” Amesisitiza Mhe Mchengerwa
Aidha, amewataka viongozi wa vilabu kuzingatia maadili na kuachana na vitendo vya ukiukaji wa maadali ambapo amefafanua kwamba vilabu haviwezi kupiga hatua katika michezo endapo havitazingatia suala hilo.
” Wenzetu wanafanikiwa sana kwenye michezo kwa kuwa wanazingatia maadili” ameongeza, Mhe. Mchengerwa
Amelitaka BMT kuchukua hatua kali kwa yoyote atakaye bainika kuvunja maadili.
Pia amesema Serikali inatarajia kujenga viwanja vya michezo ya ndani na sanaa eneo la Kawe ambapo amesisitiza baada ya kukamilika utoaji wa tuzo kwa mwaka ujao utafanyika katika kumbi hizo za kisasa.
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuifanya michezo kuwa uchumi.
Amesema kwa Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kukarabati viwanja sita nchini ambapo amefafanua kuwa lengo ni kuandaa mashindano ya soka ya AFCON.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuendeleza michezo nchini.