Mhadhiri wa lugha ya kiswahili,Dk Clara Moshi akizungumza katika maadhimisho hayo katika chuo kikuu cha Arusha leo.
Mkuu wa idara ya lugha katika chuo kikuu cha Arusha,Mushora Masija akizungumza katika kongamano hilo jijini Arusha leo.
************************
Julieth Laizer, Arusha
Arusha.Serikali imeshauriwa kuanzisha huduma mkupuo kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa watalaamu wanaoenda kuuza lugha ya kiswahili nje ya nchi katika utaratibu usiokuwa na ukiritimba na vikwazo.
Hayo yamesemwa leo julai 7 jijini Arusha na Mhadhiri wa lugha ya kiswahili ,Dk Clara Moshi wakati akizungumza katika kongamano la kiswahili katika kuadhimisha siku ya lugha ya kiswahili duniani lililoandaliwa na chuo kikuu cha Arusha .
Moshi amesema kuwa,ni vizuri serikali ikaweka mazingira mazuri ya wataalamu hao wanaoenda kuuza lugha hiyo nje ya nchi ,kwani hadi sasa hivi hatuna mfumo rasmi wa kutoa wataalamu wa kiswahili kwa ajili ya kwenda nje ya nchi badala yake mtu anajiendea mwenyewe .
Amesema kuwa, endapo kutatengenezwa utaratibu mzuri wa kufuatwa kwa wataalamu hao watakuwa wanaenda kisheria na kuweza kutambulika na ubalozi wa Tanzania na nje ya nchi kwa ujumla.
“Tuna fursa nzuri sana ya kueneza kiswahili Bara la Afrika kwani nchi zaidi ya 17 wamekuwa wakiomba wataalamu kwa ajili ya kwenda kufundisha lugha hiyo katika nchi zao ,hivyo endapo utaratibu mzuri utawekwa na serikali utasaidia sana kutangaza nchi yetu na wakitambulika kisheria kuna asilimia itatakiwa kuingia katika Baraza la kiswahili kupitia utaratibu huo “amesema.
Aidha amewataka vijana kuhakikisha wanajivua kuwa na lugha ya kiswahili ambayo inaliliwa na nchi zingine ,huku akivitaka vyuo kusisitiza umuhimu wa lugha hiyo na kuwataka vijana kuchangamkia fursa ya kuomba ajira ya kufundisha lugha hiyo nje ya nchi.
Naye Mkuu wa idara ya lugha chuo kikuu cha Arusha,Mushora Masija amesema kuwa,lugha ya kiswahili ni muhimu sana katika nchi yetu lakini changamoto iliyopo ni baadhi ya watanzania kutoidhamini lugha hiyo ambayo imekuwa ikitamaniwa na wenzetu wa nchi za nje.
Amesema kuwa,watanzania wanapaswa kudhamini na kuenzi lugha hiyo kwani ndio alama ya nchi yetu inayotutambulisha katika nchi mbalimbali huku ikiwa imebeba utamaduni mbalimbali .
Kwa upande wake Mwandishi wa vitabu ambaye pia ni Mkaguzi Msaidizi wa polisi,CCP Moshi,Salim Ng’anzi amesema kuwa,lugha ya kiswahili ni kipaji na bidhaa muhimu sana endapo kitatumiwa vizuri na kina nafasi kubwa sana ya kuikomboa jamii.
Ng’anzi amesema kuwa,alianza rasmi kuandika vitabu vya kiswahili mwaka 2019 ambapo mpaka sasa hivi ameshaandika vitabu vinne huku kimoja kijulikanacho kama ,”Mbio za Sakafuni” kikiwa kwenye mchakato wa kuingia kwenye mtaala wa elimu ya sekondari.
Mmoja wa wanafunzi chuoni hapo ,Anna Sostenesi amesema kuwa, kupitia kongamano hilo lililoandaliwa na chuo wameweza kujifunza mambo mengi sana kuhusiana na maswala ya lugha ya kiswahili na hivyo kuahidi kuongeza bidii zaidi katika masomo hayo kwa faida yao na nchi kwa ujumla.