**************
*… Jeshi la magereza laahidi kuitumia kuboresha mapato ili kutimiza adhima ya kuwalipa wafungwa*
Ikiwa ni siku chache tangu Jeshi la Magereza nchini kutangaza mpango wa kuanza kuwalipa wafungwa ili wakitoka gerezani waweze kujikimu kiuchumi. Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana Jana Julai 04, 2022 amekabidhi mizinga ya nyuki 300 kwa vikundi na taasisi mbalimbali ikiwemo Gereza la Ludewa lililoko Ludewa mkoani Njombe.
Makabidhiano haya yalifanyika mbele ya wawakikishi wa vikundi 10 kutoka kata 22 kati ya 26 za wilaya ya Ludewa pamoja na Mkuu wa Gereza Ludewa, Mrakibu wa Magereza Johannes Baitange.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mizinga 10, Mrakibu wa Magereza J.Z Baitange anasema mizinga waliyoipata itawasaidia kuboresha njia mbadala za mapato zitakazowawezesha kutimiza adhima ya jeshi hilo kuanza kuwalipa,wafungwa ili wanapotoka wawe na ujuzi na fedha kiasi cha kuanzia Maisha.
“Magereza ni taasisi inayohifadhi watu na kutoa elimu ya ulekebu kwa wafungwa, kwa elimu ya uhifadhi na ufugaji nyuki iliyotolewa leo, mimi kama msimamizi wa taasisi hii hapa Ludewa. nitaenda kuitoa elimu hii kwa vijana wangu,
“Naamini watakapomaliza kutumikia vifungo vyao elimu hii itawawezesha kujitegemea. Nashukuru leo nimepewa mizinga 10 ambapo tutakwenda ‘kusampo’ ili iwe mingi zaidi, lakini kutoa fursa ya wafungwa kujifunza kila hatua ya ufugaji nyuki, kuanzia ile hatua ya kwanza hadi ya mwisho ili watoke na ujuzi lakini pia kitu kidogo pindi watakapokuwa wanaenda majumbani mwao,” anasema Baitange.
Awali akikabidhi mizinga hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana alisema Wizara yake kwa kushirikiana na Halimashauri ya Wilaya ya Ludewa imeamua kugawa mizinga ya nyuki kwa kutambua kuwa mizinga hiyo itakwenda kusaidia makundi mablimbali ya watu katika kujitafutia uchumi.
“Tunatambua kwamba vijana na wanawake wakijikita katika shughuli za ufugaji nyuki inaongeza kipato, inasaidia kaya, familia na kadhalika. Wizara ya Maliasili na Utalii tuko bega kwa bega na wananchi wetu, tunatoa elimu ya uhifadhi na ufugaji nyuki, na mizinga hii itakwenda kuongeza kipato cha wananchi na hivyo kuachana na shughuli za uharibifu wa misitu,” anasema Mhe. Balozi Dkt Chana.
Aidha, Waziri huyo aliahidi kufuatilia kwa watu wote waliopewa mizinga hio kuona maendeleo ya ufugaji nyuki wanaofanya na kutoa wito kwa wahusika wote kuhakikisha wanatunza mizinga hiyo huku wakiwatumia wataalamu wa nyuki kutoka Wakala wa Huduma za Misitu na Nyuki nchini ambao wanaotoa elimu na ushauri wa ufugaji nyuki bure.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Andrea Tsere aliushukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa niaba ya wajasiriamali wa wilaya yake ambapo alisema mizinga hiyo itawawezesha wananchi wake kuwa na kazi mbadala ya misitu.
Kwa upande wake Afisa Nyuki. Wilaya ya Ludewa, Msemakweli Haule anasema mizinga hiyo iliyotengenezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia Shamba la Miti Sao hill haitapelekwa kwenye kata ya Manda, Luhuu, Masasi, Lupingu, KIlondo na kaya ya Lumbila kutokana na mazingira ya kata hizo kutoruhusu shughuli za ufugaji nyuki.