Na Mwamvua Mwinyi
Shule ya Kata Zogowale iliyopo Kata ya Misugusugu, Halmashauri ya Mji Kibaha imeendelea kung’ara kwenye ufaulu wa matokeo ya kidato cha sita,2022 yaliyotangazwa tarehe 5 Julai,2022 kwa kufaulisha kwa 100 asilimia.
Mkuu wa shule hiyo Tatu Mwambala amesema kuwa ufaulu umekuwa wa kuridhisha zaidi Mwaka huu kwa kupanda kutoka GPA ya 3.4 Mwaka 2021 mpaka 3.2 Mwaka huu.
Mwambala amesema kuwa wanafunzi 7 wamepata daraja la kwanza,87 daraja la Pili,78 daraja la 3 huku wanafunzi 2wakipata daraja la nne.
Mwambala ameongeza kuwa ingawa hakuna aliyepata daraja sifuri kati ya wanafunzi 174 lakini kimkoa imekuwa nafasi ya 31 kati ya shule 45 huku Kitaifa ikishika nafasi ya 592.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde, ameipongeza Idara ya Elimu Sekondari kupitia kwa Mkuu wa Idara Mwalimu Rosemary Msasi kwa usimamizi Mzuri, Walimu, Wazazi na wanafunzi wenyewe kwa mafanikio hayo na kwamba hii iwe Chachu zaidi kwa miaka mingine.
Aidha,Katibu wa tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Kibaha Marco Bahebe kando ya kuwapongeza amesema mafanikio haya yametokana na nidhamu na matumizi sahihi ya Sheria, taratibu na Kanuni.
Shule ya Sekondari Zogowale inafundisha tahasusi za HGK,HKL,CBG na PCB