Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa
Serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo bila ya kuwa na sekta
binafsi iliyoimarika.
Kauli hiyo ameitoa leo
tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam wakati akipokea nakala za Hati za
Utambulisho za Balozi Mteule wa Uganda hapa nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred
Mwesigye.
Balozi Mulamula amesema
kuwa Tanzania na Uganda zina uhusiano mzuri wa kihistoria na umekuwa ukiimarika
siku hadi siku kutokana na masuala mbalimbali ya ushirikiano yanayoendelea, yakiwemo
ziara za viongozi wa kitaifa.
Alisema kuwa hivi
karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
alifanya ziara nchini Uganda ambapo makubaliano na ahadi mbalimbali zilitolewa
katika ziara hiyo. Makubaliano hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa sekta binafsi
za nchi hizi mbili zinawekewa mazingira mazuri ya kufanya uwekezaji na biashara
kwa faida ya wananchi wake.
Alielezea matumaini
yake kuwa Balozi Mteule atahakikisha kuwa ahadi na makubaliano yaliyofikiwa baina
ya pande mbili hizo yanatekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga
unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Mhe. Waziri alimalizia
kwa kumuhakikishia Balozi huyo kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itampa
ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Balozi
Mwesigye aliahidi kuwa atatumia ujuzi na maarifa aliyopewa kwa kushirikiana na
wenzake balozini kuhakikisha kuwa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa wakati
wa ziara za viongozi wa kitaifa na majukwaa mengine yanatekelezwa ipasavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiendelea na mazungumzo na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.
|