******************************
Na. Damian Kunambi, Njombe
Wizara ya maliasili na utalii imetoa mizinga zaidi ya 300 kwa taasisi na vikundi mbalimbali vya ujasiliamali wilayani Ludewa mkoani Njombe ili kuweza kuinua uchumi wa taasisi hizo na wananchi kwa ujumla kupitia ufugaji wa nyuki.
Akikabidhi mizinga hiyo Waziri wa maliasili na utalii Balozi Dk. Pindi Chana mara baada ya kufanyika mafunzo ya uhifadhi misitu na vipimo na kusema kuwa shughuli za ufugaji nyuki zinategemea hasa misitu hivyo endapo ufugaji huo utatendeka vyema itasaidia kutunza uhifadhi wa misitu na vyanzo vya maji.
Balozi Dk. Pindi Chana asema kuwa shughuli za ufugaji nyuki zinategemea hasa misitu hivyo endapo ufugaji huo utatendeka vyema itasaidia kutunza uhifadhi wa misitu na vyanzo vya maji sambamba na kuinua uchumi wa taasisi na wananchi kwa ujumla kupitia ufugaji wa nyuki.
“Kumekuwa na uharibifu wa misitu kwa kuchoma mkaa, na matumizi mengine. Hii mizinga ina faida kubwa sana katika utunzaji misitu pamoja na kukuza uchumi kwakuwa ili uweze kufuga nyuki unatakiwa uwe na msitu wa kufugia hivyo hii itasaidia uhifadhi wa misitu yetu na kupata kipato kupitia asali” Amesema Balozi Dkt. Pindi Chana.
Aidha kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere ameishukuru wizara hiyo na kuvitaka vikundi hivyo kuitumia mizinga hiyo katika kukuza uchumi wao kwakuwa kwa sasa zao la nyuki lipo katika hali nzuri kibiashara.
Ameongeza kuwa ujio wa mizinga hiyo itakuwa msaada kwa taasisi na wajasiliamali kuwa na kazi mbadala ya misitu ambapo badala ya kukata miti ili waweze kupata kipato wataitunza ili waweze kufugia nyuki na kupata faida mara dufu.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mizinga hiyo Mkuu wa gereza la wilaya ya Ludewa Johanes Baitange ambaye ofisi yake imekabidhiwa mizinga kumi amesema mizinga hiyo itasaidia kutoa elimu ya ufugaji nyuki kwa wafungwa na pindi watakaporejea uraiani wataweza kujipatia kipato kutokana na elimu hiyo walitoipata wakiwa gerezani.