Baadhi ya wananchi wakitazama mfumo maalumu wa i Grid mara baada ya kutembelea banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar Es Salaam,
*************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya COICT, (Collage of Information and Communication Technologies) wameweza kubaini mfumo maalumu wa umeme (i Grid) unaofungwa kwenye transformer kwaajili ya kusaidia TANESCO kufahamu matatizo yanayotokea kwenye transformer.
Akizungumza leo katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar Es Salaam, Mtafiti Msaidizi wa Mradi, Bw.Nelson Kimaro amesema mfumo wa i Grid unamanufaa makubwa kwani utasaidia TANESCO katika kugundua matatizo yanayotokea kwenye transformer kwa haraka.
“Mfumo huu wa i Grid unapofungwa kwenye transformer itakuwa inaonesha ni transformer ipi na sehemu ilipo, pia itakuwa inaonesha ni tatizo la aina gani limetokea kwenye transformer na haya yote taarifa itakuwa inafika TANESCO kupitia mfumo maalumu wa kompyuta”. Amesema Bw.Kimaro.
Aidha Bw.Kimaro amesema tokea mradi huo unaanza wamekuwa wakishirikiana na TANESCO ambapo siku kadhaa walionesha sehemu walipofikia kwenye mradi huo na baadae walipewa vitu vya kuboresha zaidi na sehemu ambazo waliona kwamba zitawasaidia zaidi.
Pamoja na hayo amewataka wananchi kutembelea banda lao katika maonesho ya Sabasaba ili waweze kupata fursa kuona tafiti na bunifu mbalimbali zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam