Mkuu wa wilaya ya Nzega kamishina msaidizi wa polisi Advera Bulimba akitoa zawadi kwa mmoja ya wanafunzi walionda tuzo ya uandishi wa Insha iliyohusu mimba na ndoa za utotoni
Mkuu wa wilaya ya Nzega kamishina msaidizi wa polisi Advera Bulimba akitoa zawadi kwa mmoja ya wanafunzi walionda tuzo ya uandishi wa Insha iliyohusu mimba na ndoa za utotoni
**********************
Na Lucas Raphael ,Tabora
Wakati tatizo la ukatili wa kijinsia ,mimba na ndoa za utotoni likitajwa kushika kasi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora ,Serikali Mkoani humo imetaja kuongeza makali ya kusimamia sheria kwa wale wanaokamatwa na tuhuma za kuvunja matakwa ya haki za watoto .
Mkuu wa wilaya ya Nzega kamishina msaidizi wa polisi Advera Bulimba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora balozi Dkt. Batilda Buriani katika hafla fupi ya kuwapongeza wanafunzi walioshinda shindano la uandishi wa insha kuhusu ukatili na kupinga mimba na ndoa za utotoni.
Alisema kwamba serikali haina lelemama na wale ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya hovyo kwa watoto.
Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kusema kwamba serikali ya mkoa wa Tabora itapingana kuhakikisha Ukatili dhidi matendo ya ubakaji, ulawiti, utumikishwaji wa watoto, kunyimwa haki ya elimu, vipigo, kutopatiwa mahitaji ya msingi au kutelekezwa pale wazazi wanapotengana, kudhulumiwa mirathi na walezi vinakomeshwa ili kuweza kumlinda motto huyo.
“Wazazi wanapofariki,watoto wa kike kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo na mimba za utotoni jambo ambalo linakera sana kwani sio haki kwa mtoto kupitria madhira hayo” alisema Advera Bulimba
ACP Advera Bulimba alisema kwamba serikali itaendelea kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo ili kuhakikisha adhma ya kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili inatekelezeka kwa vitendo.
Akizungumza kwa niamba ya mkurungezi wa shirika la World Vision Esther Mongi alisema kwamba Mtoto aliyefanyiwa vitendo kikatili anaweza kupata madhara ya kisaikolojia, kimwili na kitabia,
Hivyo, kuathiri mwenendo mzima wa malezi na makuzi, kujifunza na mahusiano yake na jamii hapo baadaye atakapokuwa mtu mzima kwa kuendelea kuamini kuwa ukatili ni sehemu ya maisha.
Alisema kwamba Vitendo vya ukiukwaji wa haki za Watoto hufanywa na wazazi, walezi, ndugu waliopo katika familia, Watoto kwa Watoto, wanajamii kwa kuwapatia watoto kazi ngumu na kuwafanyia ukatili kutokana na umaskini .
Alendelea kusema kwamba baadhi ya watendaji wa Serikali, wafanyakazi katika mashirika yasiyokuwa ya serikali, na wamiliki wa migodi na Wafanyabiashara.
Alisisitiza kwamba shirika la World Vision litaendelea kupambana na mila na desturi, mabadiliko ya sayansi na teknolojia navyo vimeendelea kuwa ni visababishi vya matendo ya ukatili kwa Watoto.
Aidha kaimu mkurungezi huyo alisema kwamba shirika la World Vision Esther Mongi litaendelea kuwajengea uwezo watoto ili waweze kujiamini na kujitambua ikiwa hatua ya kukabiliana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni .
Alisema kwamba hilo linaendelea kuratibu mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za msingi ambapo katika Mkoa wa Tabora washindi wamepewa zawadi za baiskeli na fedha tasilimu huku mshindi wa kwanza kwa mkoa wa Tabora akitarajiwa hivi karibuni kwenda kushiriki mashindano hayo kitaifa Mkoani Dodoma.
Afisa maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Robert Mwanga alisema jamii inatakiwa kuwa sehemu ya kuwalinda watoto huku watoto wenyewe wakiombwa kuwa ni sehemu ya kutoa taarifa pale wanapokumbana na viashiria vya uvunjifu wa haki zao.