MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imeanzisha kanzidata (CQS) ambayo itawezesha kampuni na mtu mmoja mmoja kujisajili na kushiriki mchakato wa utafutaji na uchimbaji na mafuta nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Ushiriki wa Wazawa na Ushirikishwaji wa Wadau PURA, Charles Nyangi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 maarufu Sabasaba yanayofanyika katika Kiwanja cha Mwalimu Julius Nyerere Temeke Dar es Salaam.
Alisema PURA wameshiriki maonesho hayo ya 46 kwa lengo la kutoa elimu kuhusu fursa zinazopatikana nchini katika eneo la gesi na mafuta na namna ambavyo wananchi wanaweza kutumia kanzidata kuzitambua.
Nyangi alisema kanzidata hiyo itawezesha kila mtu anayetaka kushiriki katika eneo hilo la utafutaji na uchimbaji wa gesi kupata taarifa mbalimbali zinazowekwa na PURA.
“PURA imedhamiria kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Ila katika hawa wa ndani tunawataka watumie kanzidata ambayo kupitia makampuni yao watajisajili na CQS hiyo itawambua.
Mfano ili kupewa kazi katika eneo hilo la utafutaji na uchimbaji wa mafuta unatakiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali kama leseni, cheti ya kulipa kodi, kuandaa mahesabu na vingine, hivyo kwa sasa watakuwa wanaweka kwenye CQS, ikitokea kazi inakuwa rahisi kuona na kushindania,” alisema.
Mkuu huyo wa kitengo alisema PURA inaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa wazawa kushiriki katika kazi za uchimbaji, ununuzi, ukaratabati na nyingine ambazo zinafanyika katika eneo hilo.
Nyangi alisema kutokana na elimu na hamasa ambayo wamekuwa wakitoa kwa wazawa, hadi sasa kampuni tatu za Solution Tag, Chayil Oil Field Ltd na Ogawoga zimefanikiwa kupata zabuni katika kampuni za uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi.
Alisema baadhi ya kampuni zimepata zabuni za kufanyia ukarabati wa visima vya Kampuni ya Songo Songo ambapo zimeingiza zaidi ya Sh.bilioni 2.
Aidha, Nyangi alitoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu wakati wa Mradi wa Kuzalisha Gesi wa LNG ukianza, ambao mkataba wa awali umeshasaini kati ya Serikali na wawekezaji na zaidi ya Sh.trilioni 70 zinatarajiwa kuwekezwa.