Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19 Mheshimiwa Ted Chaiban, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 5 Julai 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19 Mheshimiwa Ted Chaiban, mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 5 Julai 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19 Mheshimiwa Ted Chaiban na ujumbe wake mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam leo tarehe 5 Julai 2022. (Kulia ni Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi)
*************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 5 Julai 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19 Mheshimiwa Ted Chaiban, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Serikali imelenga kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na Uviko 19 ikiwemo kutoa chanjo hususani kwa watu wote walio katika hatari ya kupata madhara zaidi ya ugonjwa huo.
Amesema katika kudhibiti ugonjwa huo, Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya afya, kuwajengea uwezo watumishi wa Afya katika kukabiliana na ugonjwa huo,kuimarisha huduma za dharura pamoja na ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya ili kusaidia huduma muhimu ya afya ambayo iliathiriwa na janga la Uviko19 hususani kwa huduma ya afya ya msingi.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba pamoja na mafaniko yaliopatikana katika kudhibiti Uviko19 bado serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu itakayoweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pindi yatakapotokea.
Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19 Mheshimiwa Ted Chaiban, ameipongeza Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya utoaji wa chanjo.
Amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitajika kupata chanjo ikiwemo makundi maalum kama vile watumishi wa afya pamoja na wazee.
Aidha amesema juhudi za ufanikishaji wa utoaji chanjo zinapaswa kuhusisha moja kwa moja ngazi ya mikoa na wilaya ili kufikia kirahisi malengo ya taifa katika zoezi hilo.
Pia Chaiban amesema kwamba ipo haja ya kuwaelimisha watumishi wa sekta muhimu kama vile Elimu na Utalii ili kuendelea kuhamasisha zoezi la upokeaji chanjo katika sekta zao.
Amesema changamoto za Uviko 19 zinatoa funzo kwa mataifa hususani yanayoendelea kuwekeza katika afya ya msingi pamoja na kuongeza uzalishaji wa ndani ili kuendelea kupata bidhaa hususani wakati wa mlipuko wa magonjwa duniani.