Kura za wagombea zikihesabiwa mara baada zoezi la kupiga kura lilipokamilika wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti uliafanyika jijini Dodoma
Wagombea watatu wa Skauti Mkuu Tanzania waliopendekezwa katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja. Kutoka kulia ni Rashid Mchata, Nehemia Mchechu na Aron Kagulumjuli
Wagombea wa ujumbe wa Bodi ya Skauti wakijitambulisha wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania jijini Dodoma.
Rais wa Skauti Tanzania ambae pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) akitangaza matokeo ya wagombe ujumbe wa Bodi Skauti na mapendekezo ya wagombea Skauti Mkuu wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania uliofanyika jijini Dodoma
……………………………..
Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Skauti Tanzania uliofanyika jijini Dodoma umepitisha majina matatu ya wagombea wa nafasi Skauti Mkuu ambayo yatawasilishwa kwa mlezi wa Chama hicho Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya uteuzi.
Akitangaza matokeo hayo Rais wa Skauti ambae pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amewapongeza wale wote waliogombea nafasi hiyo na kushinda na kuwataka kuendeleza mazuri ya skauti ambayo yamekwishafanyika.
Ametaja majina ya wagombea nafasi hiyo ya Skauti Mkuu yaliyopendekezwa kuwa ni Rashid Mchata, Nehemia Mchechu na Aron Kagulumjuli.
“Tunawapongeza sana kwa kupendekezwa na mkutano mkuu, na mimi kwa uaminifu napekeleka majina haya kama yalivyopendekezwa kwa mlezi ili ateue Skauti Mkuu,” amesema Prof. Mkenda
Pia Mkutano huo umechagua wajumbe wa Bodi ambao ni Elizabeth Mkwasa, Kenedy Nsenga, Juma Dossa, Jacqueline Kawishe, George Miringai, na Tabia Mohamed.
Prof. Mkenda ameitaka Skauti kuendeleza kazi nzuri iliyokwishafanyika ya kuijenga Skauti Tanzania na kuifanya kuwa imara zaidi na kwamba ili kufikia kiwango hicho ni vizuri kuendeleza tabia nzuri ya uadilifu na nidhamu.
Amesema kwa kuwa mchakato wa kumpata Skauti Mkuu unaendelea aliyepo sasa ataendelea na kazi na kuomba skauti kuendelea kushirikiana nae katika kipindi hiki ambacho atakuwa anahudumu.
Awali Waziri Mkenda aliileza Skauti Tanzania kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana matarajio makubwa kwao katika kujenga ukakamavu na uzalendo kwa vijana na kuwataka kushirikiana na kuifanya skauti kuwa imara.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Naibu Waziri Ali Abdulgulam Hussein amewapongeza wale wote walioteuliwa na kuchaguliwa na kwamba kazi iliyobaki ni kuhakikisha wanaijenga Skauti imara yenye misingi na uzalendo ndani yake.
Kwa upande wake Kamishna Mtendaji Skauti Taifa Bibi Eline Kitali amesema kwa sasa Chama cha Skauti kina wadhamini watatu ambao ni Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu Awamu ya pili, Dkt. Salim Ahmed Salim Waziri Mkuu Mstaafu, Mhashamu baba Askofu Gervas Nyaisonga na kwamba katika kuongeza nguvu amewasilisha pendekezo la nyongeza ya mdhamini Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu Awamu ya Nne jambo ambalo liliungwa mkono na skauti wote.