Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian (wa tatu kutoka kushoto) akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani wilayani Kaliua, pembeni yake aliyevaa joho ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Jafael Lufungija, Mkurugenzi wa halmashauri Jerry Mwaga na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri Abdallah Hemed, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa wilaya hiyo Paul Chacha.
……………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imekabidhi hundi ya sh mil 443.3 kwa vikundi 51 vya wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta ya kula ya alizeti na mawese.
Akiongea na gazeti hili jana Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alisema wametoa mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuviongezea nguvu vikundi vyote vyenye mwelekeo wa viwanda.
Alisema kati ya vikundi 51 vinavyokabidhiwa mikopo hiyo vikundi 18 ni vya wanawake na vitapata sh mil 128.2, vikundi 23 vya vijana sh mil 278 na vikundi 10 vya watu wenye ulemavu sh mil 37.1.
Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo sh mil 195.1 zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani na sh mil 243.2 ni fedha za marejesho ya vikundi vilivyowezeshwa awali ambavyo vimeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji.
Mwaga alibainisha kuwa katika mkopo huo sh mil 107 zimetolewa kwa vikundi vyenye viwanda vidogo vya uzalishaji mafuta ya kula ya alizeti na mawese na vinavyotengeneza chaki, viatu na sabuni ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo.
Alisisitiza kuwa dhamira yao ni kuona vikundi vya vijana, wanawake na walemavu vinaleta tija kwenye maendeleo ya wilaya hiyo kwa kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazogusa maisha ya wananchi ambazo zitauzwa ndani na nje ya wilaya hiyo na kuinua maisha yao.
Aidha aliongeza kuwa halmashauri hiyo iko mbioni kuanzisha kiwanda cha kuchakata asali na mazao mengine ya nyuki hivyo akashauri kuanzishwa kwa vikundi vingi vya wafuga nyuki ili vikopeshwe na kunufaika na fursa hiyo.
Mwaga alisema kwa sasa wametoa mkopo wa sh mil 17.3 kwa vikundi 2 vya akinamama kwa ajili ya mradi wa kuchakata asali na mazao mengine ya nyuki kupitia fedha za marejesho na mapato ya ndani.
Alibainisha kuwa kiwanda hicho kitakuwa chachu kubwa ya kuwaingizia mapato wananchi ikiwemo soko la uhakika la mazao yatokanayo na asali.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jafael Lufungija alisema wanataka kuona vikundi vyote vinavyokopeshwa na halmashauri hiyo vinafanya kazi iliyokusudiwa na kuleta tija kubwa katika uzalishaji bidhaa za chakula na biashara.
Alitaja changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili kuwa ni mwamko mdogo wa fursa za ufugaji nyuki, mitaji midogo na kutorejesha mikopo kwa wakati ila sasa elimu imeanza kutolewa na mabadiliko makubwa yameanza kuonekana.