Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba akifungua kikao kazi cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Venance Mabeyo, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba akiteta jambo na Naibu wake, Bi. Jenifa Omolo wakati wa kikao kazi cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru akizungumza na watumishi wa wizara hiyo wakati wa kikao kazi cha watumishi kilichofanyika, jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Mwenda, akifafanua jambo wakati wa kikao cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika, jijini Dodoma.
Baadhi ya wakuu wa Idara wa Wizara ya Fedha na Mipango wakifurahia jambo wakati wa kikao kazi cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika, jijini Dodoma.
Meza Kuu iliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo vya wizara hiyo wakati wa kikao kazi cha watumishi kilichofanyika katika, jijini Dodoma.
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia kwa karibu mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa kikao kazi cha watumishi kilichofanyika, jijini Dodoma.
Afisa Tehama wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jane Kazoba akichangia mada wakati kikao cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
***************************
Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, ameziagiza Idara na Vitengo vya Wizara hiyo kuhakikisha zinatimiza wajibu wake kwa ufanisi ili kuyafikia matarajio makubwa ya wananchi kutokana na mambo ambayo Serikali imejipambanua itayatekeleza kwa mwaka wa fedha 2022/23 katika kuwaletea maendeleo.
Ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa Kikao kazi cha watumishi wa Wizara hiyo ambacho kiliangazia tathmini ya kiutendaji katika kuwatumikia wananchi.
Alisema kuwa taasisi na Idara zote ambazo zinakusanya mapato nilazima kujipanga vizuri kuhakikisha mapato yanakusanywa ili kutimiza lengo la kiasi cha shilingi trilioni 41.9 kilichopangwa kukusanywa na kutumika kwa mwaka fedha 2022/23.
‘’Idara zote zinazohusika na ukusanyaji wa mapato ya ndani zihakikishe kunakuwa na usimamizi mzuri ili kazi zifanyike kwa uadilifu na kuweka mifumo madhubuti ili kuhakikisha hakuna ufujaji wa mapato ili mapato yote yakusanywe kwa wakati bila kuleta kero kwa wananchi”, alisema Bw. Tutuba
Akitoa tathmini ya utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2021/22, Bw. Tutuba alisema kuwa eneo la usimamizi wa mapato ya ndani umefanikiwa ambapo mpaka Juni mosi mapato ya jumla yamefikia takribani asilimia 96, mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania asilimia 98 na mapato yasiyo ya kodi ya Msajili wa Hazina yamefika asilimia 102.
Alisema kuwa kwa mara ya kwanza Serikali imeweza kutoa fedha za miradi ya maendeleo kufikia asilimia 86, jambo ambalo halijawahi kufikiwa kwa takribani miaka 10 na kwa upande wa fedha za matumizi ya kawaida imetoa fedha kwa mafungu yote kwa asilimia 89 ambapo kwa kipindi kirefu hali hiyo haikuwahi kufikia kwa kuwa kuna baadhi ya mafungu yamepata zaidi ya asilimia 100.
Kwa upande wao Manaibu Katibu Mkuu, Bw. Lawrance Mafuru na Bi. Jenifa Omolo, walisema kuwa Mazingira ya kufanyia kazi yamebadilika sana na yanamtaka mtumishi kufikiria tofauti kwa kuwa mahitaji ya nchi yamekuwa makubwa huku Wizara ya Fedha na Mipango ikitazamwa kama Wizara wezeshi.
Walisema mategemeo kutoka kwa Wakuu wa Serikali na viongozi wengine ni kuhakikisha Wizara inatoa majibu kwa changamoto zinazoikabili nchi hasa kwenye maeneo ya uratibu wa upatikanaji wa rasisimali fedha na usimamizi wake.
Walisema pia kazi kubwa ya watumishi wa Umma ni kuwahudumia wananchi, kwa kuwa kila kinachofanyika kwa watumishi wa Wizara hiyo kina matokea kwa Wizara nyingine na taasisi na baadae matokeo hayo yanamfikia mwananchi.
Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa na utaratibu wa kufanya tathmini kwa kuwashirikisha watumishi wake kwenye maeneo iliyofanya vizuri na yale yenye changamoto za kiutendaji kila mwaka ili kuweka mikakati bora zaidi ya kuwahudumia wananchi kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.