Baadhi ya wananchi wakipita kwa taabu kwenye daraja la miti lililojengwa kwa muda katika mto Libango baada ya daraja la awali kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Daraja la miti linalounganisha kijiji cha Libango na Mji wa Namtumbo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kama linavyoonekana kufuatia daraja la awali kusombwa na maji kufuatia mvua zilizonyesha kwa wingi mkoani Ruvuma,hata hivyo tayari serikali kupitia wakala wa Barabara za mijini na vijijini(Tarura)wameshaanza kuchukua hatua za haraka kwa kujenga daraja kubwa na la kisasa ambalo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 98.
Daraja la Libango linalounganisha kijiji cha Libango na Mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma linalojengwa na wakala wa Barabara za mijini na vijijini(Tarura)likiwa katika hatua ya mwisho kukamilika.
*************************
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
WAKALA wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,umefanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa daraja kubwa na la kisasa la Libango lenye urefu wa mita 30 lililogharimu jumla ya Sh.milioni 638,921,000.
Meneja wa Tarura wilayani Namtumbo Fabiana Lugalaba alisema,fedha hizo zilitengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kurudisha mawasiliano kwa wakazi wa kijiji cha Libango na Namtumbo ambao kwa sasa wanalazimika kutumia daraja dogo la miti kuvuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Alisema,daraja la Libango limevunjika na kusombwa na maji,kutokana na mvua zilizonyesha kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma,na kusababisha wakazi wa maeneo hayo kutumia daraja la miti ambalo sio imara na salama.
Alisema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 500,000,000 za mfuko wa jimbo na Sh.milioni 138,921,000 zinatokana na ongezeko la toso ambapo ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia tisini na nane (98) na linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai au mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Lugalaba,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Tarura shilingi milioni 838,921,000 na fedha nyingine shilingi milioni 25,000,000 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa daraja hilo.
“daraja hili litakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kijiji cha Libango na mji wa Namtumbo,mradi huu hadi utakapokamilika utatumia jumla ya Shilingi milioni 888,921,000 zilizotolewa na Serikali ya mama yetu mpendwa Samia”alisema Lugalaba.
Aidha alisema,katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetenga Sh.milioni 250,000,000 zinazotokana na ongezeko la tozo kwa ajili ya kujenga tuta kwenye maingilio ya daraja na ujenzi wa barabara kwa pande zote mbili yenye urefu wa km mbili ambapo mchakato wa ujenzi wake unaendelea.
Amewataka wananchi ambao ndiyo wanufaika wa miundombinu hiyo, kuhakikisha wanatunza daraja hilo ili liweze kudumu na liwasaidie kusafirisha mazao yao na hivyo kuondokana na umaskini.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Libango ,wameiomba Serikali kupitia wakala wa barabra za mijini na vijijini(Tarura) kumsimamia kwa karibu mkandarasi anayejenga darala la Libango aweze kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ili waweze kusafirisha mazao yao wakati huu wa msimu wa mavuno.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema,tangu daraja hilo lililopovunjika wakati wa masika maisha yao yamekuwa ya shida kwani wanashindwa kusafirisha mazao yao kwenda Namtumbo mjini kutafuta masoko au wanunuzi kwenda moja kwa moja kijiji kununua mazao.
Hassan Yasini mkazi wa Libango, ameiomba Tarura kumsimamia fundi huyo aweze kumaliza kazi haraka kwani wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kwa sababu sehemu kubwa ya maisha yao wanategemea shughuli za kilimo.
Alisema,katika msimu wa kilimo 2021/2022 wakazi wa kijiji cha Libango ambao asilimia kubwa ni wakulima wamepata bahati ya kuwa na mavuno mengi ya mazao ya chakula na biashara,lakini kutokana na changamoto ya daraja wameshindwa kusafirisha kutoka kijijini kwenda Namtumbo mjini na maeneo mengine kutafuta masoko.
Pia alisema,tangu daraja hilo lilipovunjika na kusombwa na maji mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu,kumetokea madhara makubwa ikiwamo baadhi ya watu kutekeleza na kuumia baada ya kuangukia mtoni pindi wanapojaribu kupitia kwenye daraja la muda lililojengwa kwa miti.
Mfaume Katondo mkazi wa Libango na dereva wa Bajaji alisema, kwa sasa changamoto kubwa ni namna ya kusafirisha kwani wanalazimika kushusha abiria au kumbeba mgongoni ili kumpeleka upande wa pili ,jambo linalosababisha kero kubwa kwao na abiria wao.
Hata hivyo,ameipongeza Serikali kwa kuanza kujenga daraja katika Mto Libango ambalo litakuwa mkombozi mkubwa na kurudisha mawasiliano yaliyokwama kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.
Kazembe Ponera mkazi wa Namtumbo alisema, tangu kuvunjika kwa daraja hilo changamoto kubwa ni namna ya kupata huduma na mahitaji muhimu kwa kuwa wananchi wa kijiji cha Libango wanategemea kupata mahitaji yao Namtumbo mjini ambako sasa hawawezi kwenda kutokana na ubovu wa daraja hilo.
Alisema kutokana na changamoto hiyo,sasa gharama za maisha zimekuwa juu kufuatia wafanyabiashara wamepandisha bei ya bidhaa kutokana na changamoto ya usafiri.
Msimamizi mkuu wa daraja hilo kutoka kampuni ya Jambela Ltd Dunstan Kapinga alisema, ujenzi wa daraja hilo hadi sasa umefikia asilimia 98.
Kwa mujibu wa Kapinga,muda wa ujenzi wa daraja ni miezi tisa na walianza kazi mwezi Septemba mwaka jana, hata hivyo ilivyofika mwezi Januari walilazimika kusimamisha kazi kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa wingi.
Alisema,baada ya kukatika kwa mvua wanaendelea na ujenzi na wanatarajia kumaliza kazi mwezi Julai au Agosti mwaka huu.