Mkurugenzi wa FEPT, Peter Mhagama akitoa Tamko la Taasisi ya Foundation For Environmental Protection In Tanzania (FEPT) kuhusu Loliondo na Ngorongoro,
Taasisi ya kitaifa ya Kulinda Mazingira nchini Foundation for Environmental Protection in Tanzania (FEPT) imesema inaunga mkono jitihada za serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kulinda ikolojia ya Loliondo, Ngorongoro na Serengeti isiharibiwe na shughuli za binadamu, ikiwemo ufugaji na kilimo ikieleza kuwa uwiano sahihi na matumizi sahihi ya ardhi katika maeneo hayo lazima yazingatiwe kwa maslahi mapana ya taifa.
Akitoa Tamko la Taasisi ya Foundation For Environmental Protection In Tanzania (FEPT) kuhusu Loliondo na Ngorongoro jana Mkurugenzi wa FEPT, Peter Mhagama Mkoani Arusha amesema Maliasili za taifa ni urithi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa nchini kuhusu uhifadhi wa maeneo ya Pori Tengefu la Loliondo na Hifadhi ya Ngorongoro. Sisi kama Foundation for Environmental Protection in Tanzania (FEPT), ambayo ni taasisi ya kitaifa ya Kulinda Mazingira nchini tumeguswa na mjadala huu na kuona tusikae kimya. Pori Tengefu la Loliondo lilianzishwa Mwaka 1951 na kuendelea kutambuliwa na Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 1974 likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 4,000”,amesema.
“FEPT inatoa wito kwa Watanzania wote nchini na taasisi za kimataifa za uhifadhi kuungana na serikali ya Tanzania kulinda mazingira. Umuhimu wa Pori Tengefu la Loliondo kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni mojawapo ya maeneo ya urithi wa dunia (World Heritage Site – UNESCO)”,amesema Mhagama.
Amesema Uhifadhi wa maeneo hayo ni wa muhimu ili kuinusuru ikolojia ya Serengeti akifafanua kuwa kati ya eneo zima la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000, serikali imetenga eneo la kilomita 2,500 kwa ajili ya shughuli za za wananchi, ikiwa ni sawa na asilimia 62.5% ya eneo zima.
“Eneo dogo lililobaki la kilomita za mraba 1,500 limetengwa na serikali kwa ajili ya uhifadhi kutokana na muhimu wake mkubwa sana kwa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro”,ameongeza Mhagama.
Ameeleza kuwa eneo hilo la kilomita za mraba 1,500 ni mazalia ya wanyamapori, vyanzo vya maji kwa ajili ya ikolojia ya Serengeti, mapitio ya wanyamapori wahamao kutoka Serengeti na Ngorongoro kwenda na kutoka Masai Mara, Kenya. Eneo hilo ni shoroba muhimu iliyobaki katika ikolojia ya Serengeti – Ngorongoro – Masai Mara.
“Kwa pamoja tunaweza kulinda mazingira ya Loliondo na Ngorongoro na tunazitaka jamii zote kwenye maeneo hayo kukabiliana na tishio kubwa kwa uhifadhi wa wanyamapori katika Loliondo na Hifadhi ya Taifa Serengeti linalotokana na ongezeko kubwa la mifugo”,amesema.
“Nyumbu wahama au “The Great Serengeti wildebeest migration” ni rasilimali siyo ya Tanzania peke yake, bali pia nchi jirani ya Kenya na dunia kwa ujumla. Tuzilinde Loliondo, Ngorongoro na Serengeti.Tuyalinde mazingira yetu”,amesema.
Amesema Pori la Loliondo na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro yamekuwa yakitumiwa na wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu, kama vile kilimo, ulishaji wa mifugo na makazi. Wakati maeneo ya Loliondo na Ngorongoro yakiendelea kutumiwa na wananchi, Serikali kwa upande wake imeendelea kuyatumia maeneo hayo katika shughuli za uhifadhi, ikiwemo utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
“Kama mnavyofahamu, kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu na mifugo, imeibuka migogoro mara kadhaa kutokana na wafugaji kuvamia maeneo ya uhifadhi ambayo yanalindwa na sheria za nchi”,amesema.
“Ongezeko kubwa la wananchi na mifugo, limesababisha kuharibika kwa mfumo ikolojia wa Pori la Loliondo na hivyo kuhatarisha ikolojia ya eneo hilo. Kiikolojia, Pori Tengefu la Loliondo ni muhimu kwa ajili ya kulinda Mfumo wa Ikolojia ya Serengeti, ikiwemo maeneo ya mazalia, makazi na mapito ya nyumbu wahamao pamoja na vyanzo ya maji katika mfumo huo”,ameeleza.
“Hivyo, sisi kama taasisi ya FEPT tunathamini Maisha ya watanzania wenzetu wanao ishi katika maeneo haya ya kwamba yanategemea matumizi ya rasilimali ardhi hiyo iliyowekwa kwa ajili yao kwa shughuli za kimaendeleo na tupo pamoja nao katika matumizi sahihi ya rasilimali hizo”,amesema.