Afisa mazingira bodi ya maji blonde la Pangani ,Felista Joseph akizungumza katika maadhimisho hayo jijini Arusha
Afisa afya Kenneth Twinzi akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo jijini Arusha
Wafanyakazi wa bodi ya maji bonde la Pangani wakiwa kwenye picha ya pamoja na wananchi baada ya kufanya usafi kwenye chanzo hicho cha maji kata ya Ngarenaro jijini Arusha.
…………………………………
Julieth Laizer,Arusha.
Katika kuadhimisha kilele cha wiki ya Pangani duniani , wafanyakazi wa bodi ya maji bonde la Pangani limeazimisha kwa kufanya usafi na wananchi katika chanzo cha maji cha mto Ngarenaro pamoja na kutembelea kituo cha watoto yatima cha Faraja na kutoa misaada mbalimbali.
Akizungumza leo jijini Arusha wakati wa kufanya usafi katika eneo hilo, Afisa mazingira bodi ya maji bonde la Pangani ,Felista Joseph amesema kuwa, kilele hicho kinaenda sambamba na bodi hiyo kutimiza miaka 31 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1991.
Felista amesema kuwa,wamekuwa wakishirikiana na wananchi katika kutoa elimu juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji huku na kutofanya shughuli zozote za kibinadamu katika vyanzo hivyo .
Ameongeza kuwa, wamefikia hatua ya kufanya usafi katika mto huo Kwa kushirikiana na wananchi kutokana na changamoto iliyokuwepo ya wananchi kuchafua vyanzo hivyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu na kutupa taka ngumu hali inayochangia maji kuziba katika mto huo.
“Kwa kweli eneo hili kuna uchafuzi mkubwa Sana wa mazingira unaofanywa na wananchi wenyewe kwani tumeokota taka ngumu nyingi sana katika eneo hili na wananchi wengi wanaonekana kufanya makusudi huku wakijua ni kinyume na sheria ya mazingira “amesema Felista.
Amefafanua kuwa,sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji zipo na zinajulikana ikiwemo kulipa faini kwa atakayepatikana kuvamia vyanzo vya maji ,hivyo kuwataka wananchi kufuata sheria hizo Kwa ajili ya Afya na mazingira yao kwa ujumla.
“Naombeni wananchi mshirikiane katika kutunza vyanzo vya maji na kutunza mazingira kwa ujumla ili kuondokana na magonjwa ya milipuko ambayo yanaweza kutokea kutokana na mazingira machafu na naombeni nyie wenyewe muwe mabalozi wa kuwasimamia wengine wasikiuke sheria hizo”amesema.
Naye Afisa Afya Kenneth Twinzi amesema kuwa,wamejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kuunda vikundi mbalimbali ambavyo vinalenga kusimamia swala zima la mazingira na yoyote anayekamatwa hufikishwa ofisi ya mtendaji kwa ajili ya kuchukuliwa hatua mbalimbali.
Twinzi amesema kuwa,wamekuwa wakifanya usafi kila jumamosi katika vyanzo mbalimbali vya maji ikiwa ni utaratibu waliyojiwekea ,huku akiwataka wananchi hao kutotupa taka kiholela badala yake walipie hela ya taka kwa ajili ya kuchukuliwa na gari ili kuondokana na changamoto hiyo ya uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Mmoja wa wananchi,Joyce Julius amesema kuwa, wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kutunza vyanzo vya maji ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hao kuhakikisha wanalipa hela ya taka kwa ajili ya kwenda kutupa taka zao badala ya kuzitupa kwenye vyanzo vya maji kitendo ambacho hufanya majira ya usiku.