Na Silvia Mchuruza,Bukoba
Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Karagwe ikiongozwa na Mhe. Mkuu wa wilaya ya Karagwe Mwl.Julieth Binyura ikiwa pamoja na Menejimenti ya BUWASA imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo June 30 Wilayani Karagwe inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Bukoba.
Kamati hiyo imetembelea mradi wa maji wa Omururongo-Bugene ambao una lenga kuboresha huduma kwa wakazi wa Kata ya Bugene hasa eneo la Kishao na maeneo jirani pamoja na mradi wa maji Mji wa Omururongo- Kayanga ambao ukikamilika utaboresha huduma ya maji kwa wakazi wa mji wa Kayanga ambapo miradi hii itagharimu jumla ya Tzs 1,363,477,752.88.
Aidha kamati ilitembelea miradi ya maji ya Bisheshe na Rwambaizi ambayo yote inalenga kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo ambayo mpaka kukamilika kwake itagharimu Serikali Tzs 1,331,883,432.86.
BUWASA inatekeleza miradi hiyo kupitia wataalamu wake wa ndani ambapo fedha za utekelezaji wa miradi zinagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia Mhe.Mkuu wa Wilaya ameitaka mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira BUWASA kusimamia na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wakazi wa maeneo haya waweze kupata huduma ya maji safi na salama na kuepukana na adha ya ukosefu wa maji katika wilaya hiyo.