********************************
Na Joseph Lyimo, Babati
IKIWA hivi sasa wimbi la maambukizi ya UVIKO-19 likiwa linatikisa kwenye nchi mbalimbali, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na wadau mbalimbali wa afya wamezindua chanjo zoezi la chanjo mkoani Manyara.
Wadau hao wa afya wametua Mkoani Manyara ili kusaidia kutoa hamasa ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 baada ya mkoa huo kuwa nyuma kwa utoaji wa chanjo hiyo.
Timu ya jopo hilo la wadau kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya, Shirika la JHPIEGO na Shirika la Chai wametua Manyara ili kuzindua kampeni ya utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwa awamu ya tatu.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amekiri mkoa huo kuwa chini kwenye utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 ambapo watu 33,788 ndio walipewa chanjo hadi Mei 31 mwaka huu ukilinganishwa na lengo la zaidi ya watu 600,000 waliokuwa wanatakiwa kuchanjwa.
Makongoro ameyataja malengo waliyojiwekea ili wavuke hatua hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa kuwatumia wahudumu wa afya, kuwatumia viongozi wa Serikali na kushirikiana na wadau waliopo.
“Pia, tutahakikisha tunafanya kampeni ya kuhama hama kutoka nyumba kwa nyumba, kuboresha mfumo wa utoaji taarifa na kuendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari vinavyopatikana hapa mkoani Manyara,” amesema Makongoro.
Meneja wa mpango wa Taifa wa chanjo wa Wizara ya Afya, Dkt Florian Tinuga ameeleza kuwa hadi sasa ni asilimia 21 ya walengwa wa chanjo hiyo wameshiriki kuchanjwa nchi nzima.
Dkt Tinuga anasema kwamba walilenga kuchanja watu wenye miaka 18 na kuendelea ambapo walitaka mpaka Desemba mwaka jana wawe wamefikia asilimia 70 ambalo ndilo lengo la dunia.
Ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu kuwa chanjo ipo ya kutosha hivyo wasiwe na shaka na zikipungua wadau wataleta zingine haraka.
Amezitaja sababu zilizoufanya mkoa wa Manyara kutokufanya vizuri kwenye chanjo ya UVIKO-19 ni kutokuwepo kwa wadau wa kusaidiana na jamii nyingi hasa wafugaji kuhamahama kila mara.
“Manyara mlitakiwa kuwachanja watu 956,000 ila hamjafikia hata watu 50,000 ndiyo maana tumekuja na wadau ili wasaidie kuhamasisha angalau mfike asilimia 40,” ameeleza Dkt Tinuga.
Hata hivyo, amesema baada ya kuzindua kampeni hiyo wanatakiwa kuchanja watu 200,000 kwa muda wa wiki mbili ili waweze kufikia asilimia 40 inayotakiwa hadi mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Mtaalamu huyo wa afya amezitaka halmashauri zote za wilaya zilizopo kwenye mkoa wa Manyara, kuweka mikakati itakayosaidia kuongeza idadi ya watu ambao watapata chanjo.
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt Zabulon Yoti ameeleza kuwa ili kufikia asilimia 40 ni lazima wafanye kazi na watoa huduma ngazi ya jamii na uzuri wana chanjo ya Jonsen Jonsen ambayo mtu anaipata mara moja haitaji kuirudia.
“Tufanye kazi kwa pamoja ili tufikie lengo na tutawasaidia hata baada ya kampeni hii kumalizika ili wananchi wa mkoa mzima wa Manyara, wanaostahili kuchanjwa wapate chanjo ya UVIKO-19,”amezungumza Dkt Yoti.
Kaimu Mkurugenzi JHPIEGO Dkt Mary Giatips anasema wanasaidia mikoa saba kupambana na maambukizi ya UVIKO- 19 ambayo ni Manyara, Dodoma, Singida, Zanzibar, Arusha, Kilimanjaro na Morogoro, kupitia fedha ambazo wamepatiwa na USAID.
Dkt Giatips anasema kwamba fedha zilizotolewa ni zaidi ya shilingi bilioni 1 hivyo ni vizuri zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa kupitia hamasa itakayofanywa na Mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na viongozi wengine ngazi za chini.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange anaeleza kuwa wilaya hiyo imeweka mikakati ya kuwatumia wakuu wa idara kwenda kuhamasisha zoezi la utoaji wa chanjo kila kata kuwa na mkuu wa idara mmoja.
“Kupitia hali hiyo tunatarajia wananchi wengi wa wilaya ya Babati watahamasika na kupata chanjo ili waweze kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 na kuwa salama,” anasema Twange.
Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Babati wanaeleza kuwa, Serikali iendelee kukumbusha suala la wananchi kupata chanjo kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyopo mkoani humo.
Mkazi wa mtaa wa Nyunguu Sofia Suleiman anasema kuwa wananchi wakiwa wanasikia kila wakati matangazo ya kupatikana kwa chanjo ya UVIKO-19 watashiriki ili kujikinga na janga hilo.
“Hata misikitini na makanisani, mashehe, wachungaji, mapadri na maaskofu kila mara wanawausia waumini wao waache dhambi, sasa na serikali ifanye hivyo kwa kutangaza kila mara wananchi wapate chanjo,” amemaliza kwa kusema Sofia.