Na.WAF-Tabora
Wakazi wa Tabora wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za afya pamoja na maboresho ya miundombinu kwenye hospitali za rufaa nchini
Akiongea kwa furaha licha ya majeraha alokuwa nayo Bw. Charles Uleka mkazi wa Tabora ambaye alipata ajali ya gari Tarehe 24 juni mwaka huu ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa huduma bora za Afya kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura (EMD) kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete-Tabora.
Akisimulia mkasa mzima hadi kufika Hospitalini hapo Bw. Uleka amesema mnamo siku ya ijumaa asubuhi akiwa njiani kuelekea kazini kwake kwa bahati mbaya alipata ajali iliyo sababisha mguu kuchomoka kwenye maungio ya Paja na kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Kitete akiwa hajitambui.
“Baada ya wasamalia wema kunisaidia walinifikisha katika Hospitali ya Kitete na kupokelewa katika Jengo jipya la kutolea huduma za dharura (EMD), Nilipata huduma kwa haraka na kupelekwa wodini na nashukuru hivi leo nimepata nafuu nimeruhusiwa kwenda nyumbani ” Amesema Bw. Uleka.
Bw. Uleka ameendelea kusema kuwa jengo hilo ni jengo zuri na lenye maana halisi ya jengo la kutolea huduma za dharura kwa kuwapokea na kuwahudumia wagonjwa kwa haraka.
“Mara baada ya ya kufikishwa niliweza kunyoooshwa mguu kwa haraka na kurudi katika hali yake ya kawaida, na sehemu ambazo zilikua zimechanika zilishonwa kwa haraka bila kuchelewa “.Amesema Bw. Uleka
Kwa upande wake Bi. Mektilida Lugiko Muuguzi katika kitengo cha huduma za dharura (EMD) katika Hospitali hiyo ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi katika utoaji wa huduma za Afya nchini na kupelekea kusaidia majeruhi watokanao na ajali mbalimbali kwa uharaka na ufanisi wa hali ya juu.
“Tunashukuru sana serikali kwa jengo hili linatusaidia kama watumishi kuongeza ufanisi wa kazi kutokana na mazingira yanatupa moyo na hamasa ya kufanya kazi ” Amesema Bi. Lugiko.
Serikali kupitia Wizara ya Afya ilipatiwa fedha za ahueni ya UVIKO-19 kiasi cha bilioni 263 ambazo zimeweza kujenga majengo ya kutolea huduma za dharura(EMD),kukarabati pamoja na ununuzi wa vifaa tiba kwenye hospitali za rufaa za mikoa nchini.