Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT Taifa Gaudentia Kabaka amewaomba wanawake wa Chama hicho kuendelea kumuunga mkono rais Samia Suluhu Hassan kutokana na juhudi anazozifanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mama Kabaka ametoa wito huo wakati akizungumza na wajumbe wa UWT mkoa wa Shinyanga,kupitia kikao Cha ndani kilichofanyika katika ukumbi wa Lyakale uliopo Majengo Mapya mjini Shinyanga.
Amesema rais Samia kwa kipindi kifupi ameweza kutekeleza miradi mingi ya maendeleo,ikiwemo kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Elimu na Maji.
”Tunamtetea si kwa maneno kwamba ameupiga mwingi tunamtetea kwa maelezo sahihi kila kita kila Wilaya kila Mkoa inamambo ya kumtetea Rais mama Samia Suluhu Hassan na serikali yake kuna vituo vya afya, kuna miradi ya maji najua haijaenea Nchi nzima lakini serikali inajitahidi kuhakikisha maji yanapatikana katika kila hali ambayo inawezekana miradi yote mikubwa inaendelea kwahiyo tunamtetea kwa kumsemea hata mnapokuwa na vikao waheshimiwa madiwani waambieni wale ambao hawaelewi kwenye kata zao kunanini ili inapofika 2025 wale wameshaelewa maendeleo ya Nchi hii yaliyoletwa na mwanamke wa Tanzania Samia Suluhu Hassan”. amesema Kabaka
Wakati huohuo,Mama Kabaka amewasisitiza wanawake kwa wingi kugombea Nafasi za uongozi ndani ya Jumuiya hiyo na amewataka wale wanaosimamia mchakato wa uchaguzi na zoezi la uchukuajiwa Fomu ndani ya Jumuiya hiyo kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki ili kusaidia kupatikana kwa viongozi Bora.
Amewataka wale wote wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitathimi na wawe na Nia njema ya kuleta mbadiliko chanya.
”Viongozi mliopo sasa ni wakati wa kujitafakari kujitathmini kuwa nichukue fomu au nisichukue tena lakini ninapochukua fomu lengo langu ni nini ndani ya chama na ndani ya jumuiya kwahiyo tutoke kwenye chaguzi zetu tukiwa wamoja kwa hali hiyo tusibezane, tusitukanane na kubwa tusiwekeane safu kwa sababu hizi hazina afya kwenye chama chetu mara nyingi hizi zinatubomoa nasema hivi kwa sababu uchaguzi 2024/2025 ni uchaguzi muhimu sana kwa ndani ya chama cha mapinduzi”.
Mama Kabaka pamoja na Mambo mengine,ametumia nafasi hiyo ya ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga kuwapongeza viongozi wote wa Wilaya na mkoa,kutokana na usimamizi mzuri wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa huo, mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mheshimiwa Jasinta Mboneko amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha zaidi ya Bilioni moja kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kuondoa changamoto mkoani humo.
Mboneko amesema serikali ya Mkoa wa Shinyanga inatambua na kuthmini jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo.
Amesema pamoja na mafanikio hayo bado zipo changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo changamoto ya maji ambayo inawakabili wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyamnga.
Mkuu huyo Jasinta Mboneko amesema bado ipo changamoto ya mabweni kwa wanafunzi Mkoani Shinyanga ambapo amesema serikali ya Mkoa huo kwa kushirikiana na wanawake wanaendeleo kusimamia maadili ya watoto katika makuzi ili watoto wa kike waweze kufikia ndoto zao.
Amesema serikali ya Mkoa huo inatekeleza vizuri ilani ya chama cha mapinduzi CCM kwa kuendelea kusimamia miradi mbalimbali inayoelekezwa kupitia chama hicho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Mkoa wa Shinyanga Bi. Magreth Abuoro amesema zoezi la uchaguzi kwenye Jumuiya hiyo linaendelea vizuri na kwamba matarajio uchaguzi utafanyika kwa haki.
Abuoro amesema kamati ya utekelezaji imetembelea Wilaya zote na kukutana na wanawake katika mikutano kwa ajili ya kuwahamasisha kujiunga na chama cha mapinduzi pamoja na kugombea nafasi za uongozi.
Amesema katika uchaguzi wa shina wamefanikiwa kupata mabalozi wanawake 156 na kwamba UWT Mkoa wa Shinyanga wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM mheshimiwa Samia Suluhu Hassani.
Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Shinyanga Magreth Abuoro amewahakikishia kuwa ataendelea kusimamia haki kwenye Jumuiya hiyo hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa ndani ya chama.