Mkurugenzi TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri akizungumza kwenye mkutano na wahamasishaji Jamii kudai haki zao na wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi na demokrasia Pemba kupitia mradi wa kushajihisha wanawake katika uongozi unaotekelezwa kwa mashirikiano ya TAMWA ZNZ, ZAFELA na PEGAO kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
Wahiriki wa mkutano amabao ni wahamasishaji Jamii kudai haki zao na wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi na demokrasia Pemba wakiendelea na mkutano.
Ali Othman ambaye ni mhamasishaji jamii Wilaya ya Micheweni, Akiwasilisha ripoti ya uhamasishaji jamii kudai haki zao
…………………………………………..
Na Gaspary Charles- TAMWA ZNZ
MKURUGENZI Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa amesema jamii iliyo na uwezo wa kutambua mapungufu na kubaini changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haki zao ndio msingi wa ufikiwaji fursa sawa za kimaendeleo kwa njia ya kidemokrasia katika jamii.
Alieleza kuwa jamii nyingi zinakabiliwa na matatizo mbalimbali yanayokwaza haki na maendeleo yao lakini zinashindwa kuyatatua kutokana na kukosa uwezo thabiti wa kuyazungumzia katika ngazi husika ili kufanyiwa kazi kwa wakati.
Dkt. Mzuri alieleza hayo wakati akizungumza na wahamasishaji Jamii kudai haki zao na wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi na demokrasia Pemba kupitia mradi wa kushajihisha wanawake katika uongozi unaotekelezwa kwa mashirikiano ya TAMWA ZNZ, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway Nchini.
Alifahamisha kwamba iwapo jamii itakuwa na uwezo wa kuyaibua matatizo yanayowakabili na kuchukua hatua sahihi itasaidia kuchochea uwajibikaji katika upatikanaji wa haki zao.
Mapema mkurugenzi huyo alihimiza wahamasishaji jamii hao ambao wanafanya kazi katika Wilaya zote nne za Micheweni, Wete, Mkoani na Chake Chake kisiwani Pemba kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kuwasaidia wananchi kuwa na uwezo wa kuibua matatizo yanayowakabili na kuyataftia ufumbuzi kwenye vyombo husika.
“Dhana ya mradi kuunda wahamasishaji jamii ni kuhakikisha yule mwananchi wa chini awe na uwezo wa kuyaibua matatizo yanayomkabili, kisha aweze kuchukua hatua dhidi ya matatizo hayo na kuwa na ujasiri wa kukaa meza moja na mamlaka husika kutafta ufumbuzi kwa njia ya demokrasia,” alisema Mzuri.
Aidha alieleza kuwa uwepo wa wahamasishaji hao katika jamii unalenga kuwafanya watoa huduma wa taasisi mbalimbali kuongeza kasi ya uwajibikaji dhidi ya utatuzi wa vikwazo vinavyowakabili wananchi kwenye maeneo yao.
Alieleza, “majukumu makubwa ya wahamasishaji jamii ni kuwafanya watoa huduma wafanye kazi zao vizuri kwa uwazi, na wawajibike kwa wananchi ipasavyo, na huo ndio msingi haswa wa dhana ya utawaka bora.”
Kutokana na wanawake kukosa misingi imara ya uelewa katika masuala mbalimbali yatakayowajenga kwenye nafasi za uongozi, aliagiza wahamasishaji hao kuangalia uwiano wa usawa wa kijinsia ndani ya kamati za shehia ili kutoa fursa sawa kwa wanawake kutokana na huko ndipo msingi wa uongozi unapoanzia.
Akiwasilisha ripoti ya uhamasishaji jamii kudai haki zao, Ali Othman ambaye ni mhamasishaji jamii Wilaya ya Micheweni, alieleza kupitia mikutano iliyofanyika kwenye shehia mbalimbali walibaini kuwepo baadhi changamoto ikiwemo uelewa mdogo wa wanawake katika masuala yatakayowasaidia kuingia kwenye nafasi za uongozi jambo ambalo linakwamisha ushiriki wao kikamilifu katika nafasi hizo.
Aidha alibainisha changamoto nyingine ni uwepo wa vyeti feki vya kuzaliwa kwa baadhi ya wananchi wa Shehia ya Shumba, Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba, jambo ambalo linapelekea wananchi wengi kukosa haki zao za msingi ikiwemo nafasi za uongozi.
“Tatizo la uwepo wa vyeti feki vya kuzaliwa kwa wakaazi wa Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ni moja ya changamoto kubwa tuliyoibua kwenye jamii, kwani katika mikutano yetu kwenye shehia wananchi wengi hasa Shehia ya Shumba Mjini kilio chao ilikuwa ni kupata vyeti feki,” alieleza mhamasishaji huyo.
Aidha alifahamisha kuwa uwepo wa wahamasishaji hao katika jamii umesaidia kujenga uwezo kwa jamii kuwa na uthubutu wa kuzungumza matatizo yanayowakabili kwa uwazi.
Nae Husna Khamis kutoka Wilaya ya Wete alieleza, baada ya kubaini kuwepo kwa tatizo la kutojua kusoma na kuandika kwa wananchi wengi hasa wanawake, walishirikiana na jamii kuanzisha madarasa ya watu wazima ili kuwapatia fursa wananchi kuondokana na tatizo hilo linalowakosesha haki zao muhimu.
Alisema, “kupitia uhamasishaji kwenye shehia, tumefanikiwa kuzindua madarasa 6 ya watu wazima yakiwa na jumla ya watu 130 kwaajili ya kuwawezesha kusoma na kuandika katika Shehia ya Mlindo, Wilaya ya Wete na tayari wengi wao wameshaanza kujua kusoma na kuandika.”
Mapema afisa tathimini na ufuatiliaji wa ZAFELA, Rajab Hamad, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na wahamasishaji hao kwa kufanikisha ufuatiliaji wa changamoto na vikwazo vinavyo chelewesha upatikanaji wa haki za wananchi.
“Niwapongeze sana wahamasishaji jamii Pemba kwa kufanikisha ufuatiliaji wa changamoto za wananchi na kuhakikisha zote tulizofuatilia zinakuwa na matokeo chanya kutokana na ufuatiliaji mliofanya kwenye ngazi mbalimbali, na hii ni kwasababu kwamba lengo la mradi huu wa SWIL sio tu kuibua matatizo ya wananchi ila ni kusaidia kushirikiana na jamii kutafta ufumbuzi wa matatizo hayo.”
Mradi wa kushajihisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na demokrasia ni mradi wenye lengo la kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi ambao unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway Nchini.