Waziri wa maji ,Jumaa Aweso akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo jijini Arusha leo.
Mkurugenzi wa idara ya usambazaji maji na usafi wa mazingira wizara ya maji, CPA Joyce Msiru akizungumza katika mafunzo hayo.
Katibu Mkuu wizara ya maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza katika mafunzo hayo .
**************************
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha.WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amewaagiza Wakurugenzi na wenyeviti wa Bodi za maji nchini kuhakikisha wanadhibiti suala la wananchi kubambikiziwa bili za maji (Ankara za maji) za mifukoni mwa baadhi ya watumishi wasio na uadilifu na kuzua malalamiko mengi kwa wizara.
Akizungumza Leo jijini Arusha jijini wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Bodi na Menejimenti za Mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini,Aweso amesema hiyo imekuwa kero kubwa ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wizara.
“Nawaombeni sana wakurugenzi na wenyeviti wa bodi mkadhibiti changamoto hiyo kwani wananchi wengi wanabambikiziwa bili za mfukoni na siyo zile zilizopo kisheria za EUWRA,”amesema.
Aweso amesema kuwa,wananchi wanatakiwa kupewa bili zile tu zilizopitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EUWRA na siyo vinginevyo.
Ameongeza kuwa,ni vema wakahakikisha wananchi wanaelewa Teknolojia ya kisasa ya ulipaji maji ( Pre-Paid Meter) ili kuondoa malalamiko hayo.
Aweso amesema kuwa, serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kupitia miradi unaotekelezwa nchini,lakini baadhi ya maeneo inasikitisha kusikia wananchi wakiomba kuunganishiwa maji inachukua miezi mitatu kupewa huduma hiyo.
“Fuateni maagizo ya serikali mtu akiomba kuunganishiwa maji haitakiwi kuzidi siku saba awe amepata huduma hiyo sasa nashangaa kuna wananchi wanakaa hadi miezi mitatu hawajapata maji naombeni sana msimamieni na mchukue hatua kwa baadhi ya watumishi wanaoshindwa kutekeleza swala hilo,”amesema.
Naye Katibu Mkuu wa wizara ya maji Mhandisi Anthony Sanga ameitaka bodi ya wakurugenzi kuwa na utaratibu wa kukaa vikao na watumishi wake ili kubaini kero kwa wakati pamoja na kuchukua hatua kwa wakati pale zinazojitokeza .
Amesema kuwa,wizara hiyo inapitia Mapinduzi makubwa kwani imekuwa wizara ya utatuzi wa changamoto za maji na kuondoka kwenye wizara ya malalamiko.
Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya maji CPA Joyce Msiru amesema kuwa, mafunzo hayo yameshirikisha washiriki 145 ambapo mada 12 zitawasilishwa kwenye mafunzo hayo.
Ametaja lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kuongeza uelewa kwa watendaji hao ili wasimamie utoaji wa huduma bora za maji kwa wananchi.