Afisa Wanyamapori wilaya ya Tunduru Limbega Hassan akitoa taarifa ya matukio ya wanyamapori waharibifu kwa Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro(hayupo pichani)aliyetembelea ujenzi wa kituo cha askari wa wanyamapori kinachojengwa katika kijiji cha Chingulungulu kata ya Muhuwesi.
Kaimu Mkuu wa idara ya maliasili na mazingira wilaya ya Tunduru Omben Hingi akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo cha askari wa wanyamapori kwa Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro wa pili kushoto kinachojengwa katika Chingulungulu wilayani humo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro akizungumza na viongozi wa kijiji cha Chingulungulu na kata ya Muhuwesi alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha askari wa wanyamapori katika kijiji cha Chingulungulu wilayani humo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro, akisikiliza maelezo ya ujenzi wa kituo cha askari wa wanyamapori kutoka kwa fundi wa mradi huo Shaban Allai wakati mkuu huyo wa wilaya alipotembelea kuangalia ujenzi wake.
Picha zote na Muhidin Amri
………………..
Na Muhidin Amri,
Tunduru
SERIKALI kupitia mamlaka ya usimamizi wanyapori Tanzania(Tawa) kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya Tunduru,imeanza kujenga kituo kikubwa cha askari wa wanyamapori ili kudhibiti wanyama wakali na waharibifu wanaovamia makazi ya watu na kuharibu mazao mashambani.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa idara ya maliasili na hifadhi ya mazingira wilaya ya Tunduru Ombeni Hingi,kwa mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro aliyetembelea ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa katika kijiji cha Chingulungulu kata ya Muhuwesi.
Hingi alisema,lengo la kujenga kituo hicho ni katika jitihada za Serikali za kudhibiti na kukabiliana na changamoto kubwa ya wanyama hao hasa Tembo wanaotoka porini na kwenda kwenye makazi ya watu.
Alisema,wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto kubwa ya wanyama wanaohatarisha maisha ya watu na kuharibu mashamba,hivyo Serikali imeona ni vyema kujenga kituo hicho ambacho kitakuwa na askari watakaofanya kazi ya kudhibiti wanyama hao.
Kwa mujibu wa Hingi,walifanya jitihada mbalimbali kuomba msaada katika taasisi,idara za Serikali na zisizo za Serikali ili kuwasaidia kukabiliana na wanyama hao,lakini wizara ya maliasili na utalii kupitia Tawa ndiyo waliokubali kutoa Sh.milioni 80 kwa ajili ya kujenga kituo hicho.
Alisema,kwa sasa Halmashauri ya wilaya Tunduru kupitia idara ya maliasili inakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendea kazi na watumishi ambao wako tisa(9) tu hivyo ,hawawezi kutokana na tatizo kubwa la wanyama hao katika wilaya ya Tunduru.
Alisema,kujengwa kwa kituo hicho na vituo vingine vidogo vitakavyojengwa hapo baadaye ambavyo vitakuwa na askari wengi kutaongeza nguvu katika jitihada za kukabiliana na wanyamapori.
Kwa upande wake Afisa Wanyamapori wa wilaya hiyo Limbega Hassan alisema,kijiji cha Chingulungulu na kata ya Muhesi ni maeneo yenye changamoto kubwa ya kuvamiwa na wanyamapori mara kwa mara.
Alisema,kujengwa kwa kituo hicho katika kijiji hicho ni kama bahati kwani kuna maeneo mengi yenye uhitaji wa askari wa wanyamapori na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa askari watakaoletwa ili waweze kutekeleza majukumu yao badala ya kuwaogopa.
Diwani wa kata ya Muhuwesi Imani Ngonyani amehaidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa fundi aliyepewa kazi ya kujenga kituo hicho na hata kwa askari watakaoletwa kwa ajili ya kusaidia wananchi kukabiliana na wanyama hao.
Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa usikivu wake na kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Tunduru katika kudhibiti matukio ya kushambuliwa na Tembo.
Alisema,tatizo la wananchi kushambuliwa na tembo katika maeneo yao limekuwa kubwa kutokana na wilaya hiyo kwa sehemu kubwa kuzungukwa na Hifadhi ya Nyerere yenye wanyama wengi wakali na waharibifu wa mazao.
Ameitaka idara ya maliasili wilaya,kuendelea kuomba na kutafuta fedha kwa wahisani mbalimbali ambao watasaidia kuendelea kujengwa kwa vituo vingine katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa ajili ya makazi na ofisi za askari wa wanyamapori.
Alisema, kituo hicho ni mwanzo tu na kuhaidi kuwa serikali ya wilaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kujenga vituo vingi vya askari ili kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
“nimekaa Tunduru miaka mitatu sasa natambua ukubwa wa tatizo la Tembo,hatuwezi kuwaacha wananchi wanaendelea kufa na mazao yao yanaliwa, sisi kama viongozi tuliopewa dhamana ni lazima tuanze kutafuta suluhu ya matatizo ya wananchi wetu bila kutegemea serikali kuu”alisema Mtatiro.
Amemwagiza fundi kuhakikisha anawatumia vijana wanaotoka katika eneo hilo katika ujenzi wa kituo hicho,badala ya kuwatumia vijana kutoka nje ya kata hiyo na kuwashukuru viongozi wa vijiji na kata kwa uamuzi wa kutoa ardhi bure.