PICHA mbalimbali za matukio ya ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alipotembelea baadhi ya miradi ya barabara zinazotekelezwa na TARURA pamoja na nyingine TANROADS Kibaha Mjini, Mkoani Pwani.
………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, amesema kwa hakika Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,imeitendea haki Wakala wa barabara za Vijijini na mjini (TARURA )kwa kutenga fedha za utekelezaji wa miradi kiasi cha sh Bilioni 44.650.6 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Kati ya fedha hizo Bilioni 21 .111.6 Ni kwa ajili ya mradi wa barabara ya lami Visiga -Zegereni na Bilioni 1.367.387.2 kwa Ajili ya miradi ya dharura Kibiti , Mkuranga,Kibaha na Bagamoyo.
Akikagua miradi ya barabara Viuatilifu,TAMCO -MAPINGA ambayo ipo chini ya TANROADS , barabara ya kuelekea hospital ya Lulanzi,Tanita kuelekea chuo cha uongozi cha CCM na Visiga -Zegereni , Kunenge aliwataka wakandarasi wazitendee haki fedha hizo nyingi zinazotolewa na Serikali kwa kutekeleza miradi kwa wakati bila ubabaishaji .
“Fanyeni kazi usiku na mchana, kama umepewa tenda ya kuwa mkandarasi manake umeaminiwa, tekelezeni kazi kwa wakati na kama kuna vikwazo mnijulishe,:Sitaki kusikia changamoto ya mvua kwani wakati unapewa tenda hii hamkujua kama kuna mvua!?alihoji.. Kunenge
Mmeaminiwa onyesheni uwezo wenu.
Alieleza ,TARURA na TANROADS Wana mahusiano mazuri ya kiutendaji kazi wanafanya kazi kubwa ,ambapo kwa TARURA imeshapelekewa asilimia 95 ya fedha zote.
Kunenge alifafanua,kwa TANROADS ilitengwa zaidi ya sh.bilioni 42 na Hadi Sasa wameshapelekewa asilimia 75 ya fedha hizo.
“Tunamshukuru Rais wetu,mkoa kautendea haki ,Kwa upande wa barabara hii ya Visiga -Zegereni Ni mradi unaokwenda Viwandani km 12.5 unatekelezwa na TARURA ,Sasa utaona mradi huu unagharimu Bilioni 21 Hadi kukamilika Ni Jambo la faraja kwakuwa utasaidia wawekezaji kusafirisha malighafi na bidhaa zao kwa urahisi”alisisitiza Kunenge.
Awali Meneja wa TARURA mkoa ,Leopold Runji alisema mradi wa Visiga- Zegereni umefikia asilimia 10 Hadi Sasa.
Alisema ,wametengewa Bilioni 44.6 na wameshapokea Bilioni 25.074.3 .
Runji alitaja mafungu ya fedha walizopokea kimkoa Kuwa ni Pamoja na mfuko wa barabara Bilioni 8.2 kwa Ajili ya matengenezo ya barabara ya kawaida kilometa 873.98 , Mfuko wa Jimbo Bilioni 4.8 na Miradi ya fedha za tozo Bilioni 28.236.6 .
Dereva bodaboda Majid Muhammad alisema kwasasa wanapata changamoto kipindi cha mvua hivyo wanashukuru Serikali kwa mipango ya kuboresha barabara Hali itakayowawezesha kupita kwa urahisi .