Mgeni Rasmi katika warsha hiyo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akiwa meza kuu pamoja Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa sheria kutoka NEMC Injinia Redempta Samuel (katikati) aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC pamoja Meneja wa NEMC Kanda ya Nyanda za juu Kusini Bi Glory Kombe (wa kwanza kushoto)Mgeni Rasmi katika warsha hiyo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe waliohudhuria warsha kuhusiana na usimamizi wa taka hatarishi na za kielektroniki iliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa mkoani MbeyaMkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ambaye alikua Mgeni Rasmi katika warsha ya wadau wanaojishughulisha na taka hatarishi kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya
Sehemu ya Wadau walioshiriki katika warsha iliyoandaliwa na NEMC kwa Wadau wanaojishughulisha na taka hatarishi kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.
***************
Suala la Mazingira ni suala mtambuka ambalo linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kuyalinda mazingira yetu kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadae. Mazingira tunayoishi sasa ni urithi na tumeyaazima kutoka kwa vizazi vijavyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ambaye alikua Mgeni Rasmi katika warsha ya wadau wanaojishughulisha na taka hatarishi iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya ikihusisha wafanyabiashara kutoka katika Mikoa ya Mbeya,Songwe, Njombe na Iringa .
Alisema kuwa Wadau wanaojishughulisha na taka hatarishi ama kwa kukusanya, kuhifadhi, kusafirisha au kurejereza wanalo jukumu la kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao vema ili kuweza kulinda mazingira na uchumi wa nchi kupelekea kuwa na maendeleo endelevu.
“Taka hatarishi ziko za aina nyingi ikiwemo kemikali za viwandani, vifaa vilivyochakaa vya majumbani, migodini, betri chakavu,oili iliyotumika, chuma chakavu na taka za kielektroniki hivyo ni jukumu letu kuweza kulinda mazingira na kuyatunza”.
Aidha ameongeza kuwa Tanzania biashara ya taka hatarishi imegawanyika katika makundi makubwa mawili. Kundi la kwanza ni la wafanyabiashara wadogo wanaotumia vibanda kama sehemu za kuhifadhia kwa muda na kuajiri vijana wanaopita mitaani na matoroli au mabegi wakikusanya taka kutoka kwenye makazi, maofisini na viwandani.
Kundi la pili ni la wafanyabiashara wakubwa wanaokusanya kwa lengo la kusafirisha nje ya nchi au kutumia kwenye viwanda vya kurejereza kama malighafi kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali kama vile nondo.
Vilevile Mkuu wa Mkoa ameipongeza NEMC kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kusimamia utunzaji na uhifadhi wa mazingira likiwemo suala la upatikanaji wa vibali kwa urahisi na mapema.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza sana NEMC kwa kujitahidi kitoa vibali mapema na kwa wakati hii inasidia sana kurahisisha utendaji kazi kwa Wawekezaji hapa mkoani Mbeya”
Naye Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa sheria kutoka NEMC Injinia Redempta Samuel akisoma hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC ambaye alimwakilisha amesema kuwa kutokana na utandawazi na teknolojia kumekua na ongezeko kubwa la shughuli za kurejeleza taka hatarishi hapa Nchini hivyo kupelekea NEMC kuandaa warsha hiyo ili kuweza kutoa elimu, kukuza uelewa na kubaini pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara katika kutekeleza matakwa ya sheria.
“Ni matumaini yetu kuwa baada ya mafunzo haya , Wadau wote waliohudhuria hapa wataweza kufanya shughuli zao za biashara ya taka hatarishi bila kuvunja sheria na kupunguza athari za kimazingira na kijamii zinazotokana na shughuli za biashara za taka hatarishi.
Nao Wadau wanaojishughulisha na taka hatarishi walioshiriki katika warsha hiyo wameishukuru NEMC kwa kuandaa warsha hiyo na kuweza kuwajengea uelewa, kuwapa elimu pamoja na kuwapatia fursa kuuliza maswali mbalimbali yaliyokua yanawatatiza na yakapatiwa ufumbuzi. “Tunaishukuru NEMC kwa kuandaa warsha hii ambayo imekua msaada kubwa kwa sisi kupata uelewa na kufahamu mengi ambayo tulikua hatuyajui”