Na Magreth Kinabo – Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma amewasihi wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kupitia wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi na wadau wote katika mnyororo wa haki, kutambua kuwa jukumu la utoaji haki ni sehemu muhimu ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Akizungumza leo Juni29, mwaka huu katika mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo wa siku mbili unaoendelea katika ukumbi wa LAPF jijini Dodoma, Jaji Mkuu alisema utekelezaji wa wajibu wa wafanyakazi hao ni katika utoaji haki unaimarisha utawala wa sheria na pia utawala bora.
“Utekelezaji wa wajibu wenu unachangia pia uwepo wa amani ya nchi, na huimarisha uchumi na ustawi wa Watanzania. Kila Mtumishi wa Mahakama atambue kuwa yeye ni sehemu ya mnyororo wa utoaji haki. Unapotimiza wajibu wako kikamilifu na kwa uadilifu, mnyororo wa haki unakuwa imara na kufanikisha uwekezaji na pia shughuli za biashara za ndani na za kimataifa.” Alisema Prof. Juma
Aliongeza kwamba hata watalii wanaongezeka kutokana na kazi nzuri ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia mkakati wa ‘Royal Tour’, wanafurahia kuja Tanzania kutokana na kuwepo kwa amani ambayo inatokana na watumishi waadilifu katika mnyororo wa utoaji Haki.
Alisema kila mtumishi wa Mahakama inabidi afahamu mwelekeo na Dira ya Mahakama. Hivyo wajumbe hamna budi kuendelea kuwaelimisha watumishi wote wapi Mahakama ya Tanzania inapoelekea.
Aliishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyowezesha kwa hali na mali na ambavyo inatoa kipaumbele kwa mahitaji ya Mhimili wa Mahakama, ambapo hivi karibuni Serikali ya Tanzania imechukua tena Mkopo wa gharama nafuu wa dola za Kimarekani milioni 90 (zaidi ya bilioni Tsh 210) kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu ya Mahakama Tanzania kwa mwaka ujao wa Fedha 2022/23.
“Ni vyema mkafahamu kuwa katika jitihada za kuhakikisha mfumo matumizi ya fedha ni imara, nimejulishwa kuwa, katika ujenzi wa vile Vituo 6 Jumuishi, baada ya vipimo vya mwisho (re-measurement), tumeweza kuokoa zaidi ya bilioni Tsh 3.5. Fedha zilizobakizwa kwenye ujenzi zimetumika kununulia vitendea kazi vingine ambavyo vitazidi kumarisha ufanisi wetu katika utoaji haki,’’alisema.
Alisema kutokana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia wafanyakazi wote wa Mahakama na wadau wetu, kutokubali kubaki nje ya Mradi Mkubwa wa Serikali ukiwepo mradi mkubwa uitwao TANZANIA YA KIDIJITI (Tanzania Digital Project) iliyoanza mwaka jana (2021).
Alifafanua kwamba ni wajibu waw a Mwajiri namna kutoa huduma kuweka kuweka programu za mafunzo endelevu ambayo yatawawezesha wafanyakazi wa kada zote kuhama kutoka utoaji huduma kwa njia 13 zilizozowekwa hadi kutoa huduma katika Mahakama ya Kidijiti au Mahakama Mtandao. Huku akikitaka Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), kutafakari mafunzo hayo maalum.
”Katika kutekeleza hili hata maeneo ya pembezoni yapewe kipaumbele na siyo maeneo ya mijini tu. Ni muhimu sote tuwe kwenye safari moja na asiwepo atakayeachwa nyuma eti kwa kuwa yuko kwenye Mahakama ya maeneo ya vijijini, ikiwemo kuwashirikisha wadau kwenye suala hilo, alisisitiza.
Aidha Jaji Mkuu huyo amlimtaka kila mtumishi kutafuta maarifa ili kuweza kuwa mtumishi bora kwa kuwa hakuna wakati maarifa yanatosha.
Kwa wale ambao wako karibu na vyuo vya elimu ya juu vinayotoa masomo ya jioni ni vyema kuanza kuchangamkia fursa hii kuanzia Majaji, Mahakimu, watendaji na watumishi wasaidizi.
Jaji Mkuu amewataka watumishi hao kujitokeza siku ya Sensa tarehe 23 Agosti 2022 ili kushiriki zoezi la kuhesababiwa.
Jaji Mkuu pia alisema ugonjwa wa UVIKO bado upo kwa viwango vinavyobadilika hivyo aliwataka wale ambao hawajapata chanjo kuenda kuchanja.