*************************
NJOMBE ,
Wakazi wa kijiji cha Mahongole kilichopo halmashauri ya Mji wa Makambako wilayani Njombe Wameitaka serikali kuwasaidia kupata ardhi yao yenye ukubwa wa ekari 1001 iliyochukuliwa na muwekezaji wa kigeni kutoka Kampuni ya DL Group ama kulipwa fidia ya kupisha maeneo hayo ambayo waliayatoa baada ya muwekezaji huyo kukiahidi kijiji kujenga Bandari Kavu na viwanda vya kuzalisha nguo,chuma na parachichi.
Wakazi hawa wanasema 2019 muwekezaji huyo kutoka Kenya alifika kijijini kwao kuomba ardhi ya kuwekeza viwanda na kisha kuahidi kulipa fidia lakini hadi sasa inaelezwa ni ekari 371 tu zilizolipwa fidia jambo ambalo limezidi kuongeza umasikini kwa familia zizilizopisha mradi huo kwa miaka mingi bila kufanya uzalishaji.
Kufuatia changamoto hiyo waliyokiri kuwarudisha nyuma kimaendeleo Wakazi hawa akiwemo Chesko Sambala,Mussa Kindole na Laurent Mlelwa wanatumia mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu wa wilaya ya Njombe wenye lengo la kusikiliza kero za wananchi kuomba serikali kuwasaidia kupata maeneo yao ama fidia ya fedha kwasababu tangu muwekezaji achukue ardhi hiyo miaka minne iliyopita ametoweka na hakuna ujenzi wa viwanda na bandali kavu unaofanyika kama walivyoelezwa.
Mara baada ya kusikia kero hiyo na ukubwa wa eneo lililochukuliwa kwa zaidi ya miaka 4 bila kuendelezwa ndipo mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa Kasongwa akaomba kupewa wiki mbili kulifuatilia sakata hilo huku diwani wa kata ya Mahongole Mario Kihombo Akisema uharaka unatakiwa Katika kutatua mzozo huo.
Katika mkutano huo wananchi wengine akiwemo Petro Nathan,Jimson Salinhwa na Omary Diwani Mkuu wa Polisi Makambako wameweka bayana changamoto nyingine ambazo ni Vitambulisho vya NIDA,uhalifu na umeme.