***************************************
Na Joseph Lyimo
PAMOJA na kuwa maambukizi ya virusi vya UVIKO-19 yaliwakumba baadhi ya watu na wengine kupoteza maisha yao, bado kuna vijana wengi walichangamkia fursa ya ugonjwa huo na kujinyanyua kiuchumi kwa kutengeneza barakoa na vitakasa mikono.
Baadhi ya vijana wa mkoa wa Manyara, walihamasika kuunda vikundi na kutengeneza barakao hizo na kuziuza maeneo mbalimbali ikiwemo mahosipitalini, kwenye nyumba za ibada, sokoni na minada na kwenye machimbo ya madini.
Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa tamko la kukubali matumizi ya barakoa zilizotengenezwa nchini na siyo zilizotoka nje pekee ili mradi zikidhi masharti yaliyotolewa ikiwemo mazingira ya usafi.
Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Eva Mathayo ambaye alikuwa anajishughulisha na ufundi wa cherehani anasema alitengeneza barakoa na kuwauzia watu mbalimbali ili kujikinga na UVIKO-19.
“Watu wengi walipenda bei zetu kwani barakoa moja tulikuwa tunauza shilingi 500 na tukapata soko zuri kwani walipenda huduma yetu,” anaeleza Eva.
Anasema mafundi wengi waliingiza kipato kutokana na kushona barakoa kwa kutumia vitambaa ili watu wajikinge na maambukizi ya UVIKO-19.
“Japokuwa baadhi ya watu walikuwa wanadharau barakoa hizo tulizokuwa tunazishona ila sijawahi kupata malalamiko hata kwa mtu mmoja kuwa amevaa barakoa niliyoshona na akapata madhara ya UVIKO-19, mafua au kukohoa,” anaeleza Eva.
Fundi wa kushona nguo wa mji mdogo wa Kibaya Wilayani Kiteto, Khamis Ally anasema alitengeneza barakao na wateja wake wengi walikuwa ni wajasiriamali wa soko, wakulima na wafugaji mbalimbali waliokuwa wananunua kwa shilingi 500.
Fundi huyo anaeleza kuwa walipata mafunzo ya muda mfupi kupitia idara ya afya kwenye hospitali ya wilaya ya Kiteto, juu ya namna ya kutengeneza barakoa hizo.
Mkazi wa mjini Babati ambaye anafanya kazi ya kuuza samaki kwenye soko kuu la eneo hilo Sofia Athuman anasema baada ya kupatikana kwa fursa za barakoa za vitambaa vilivyokuwa vinashonwa na mafundi, ilikuwa nafuu kwao kwani wataalam wa afya walitoa masharti kwa barakao za awali kutumika kila baada ya saa mbili au nne na kisha kutumia nyingine.
“Hali ya uchumi kwa sisi watanzania wa hali ya chini ni ngumu kwani hatungeweza kuwa na barakoa zile zinazouzwa kwenye maduka ya dawa ambazo kwa siku unapaswa kutumia zaidi ya nne kwani zinavaliwa kwa masaa,” anasema.
Anasema barakoa za kwenye maduka ya dawa zilikuwa zinauzwa kati ya shilingi 1,000 hadi shilingi 2,000 na zinavaliwa kwa masaa kadhaa na barakoa za vitambaa vilikuwa vinauzwa shilingi 500 na unavaa na kufua jioni ndiyo sababu watu wengi wakakimbilia hizo.
Hata hivyo, mratibu wa UVIKO-19 wa Wilaya ya Babati, Dkt Emmanuel Mkony anasema vijana wameweza kujipatia fursa ya ajira kwa kutengeneza barakoa na vitakasa mikono ila baadhi yao walitengeneza barakoa hizo nyingine hazina viwango vya ubora ambavyo vinahitajika.
Dkt Mkony anaeleza kuwa baadhi ya barakoa hizo malighafi zilizotumika hazikupitisha na Wizara ya Afya na ikiwemo vitakasa mikono vingine vilivyokuwa vinatumika kunawa mikono.
“Baadhi ya watu walilalamika kupata madhara ya kiafya ikiwemo kubabuka mikono, kuumwa vichwa, kupata mafua na kukohoa hivyo jamii inapaswa kutumia vitu ambavyo vimepitishwa na wataalam wa afya,” anasema.
Kwa upande wake mkazi wa mjini Babati Yusuf Juma anasema kupitia maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 alichangamkia fursa ya kuuza malimao kwa baadhi ya watu waliokuwa wakijikinga na maradhi hayo.
Anaeleza kwamba bei ya malimao ilipanda mara dufu kutokana na matumizi yake kuongezeka ikiaminika kuwa ukipata mchangamnyiko wa limao na tangawizi, UVIKO-19 itatoweka.
“Biashara ilikuwa nzuri kwani limao moja lilifika hadi shilingi 500 kutoka shilingi 100 ya awali, yaani machungwa yalikuwa yana soko kubwa kuliko limao ila hivi sasa limao ndiyo linaonekana la maana kuliko machungwa,” anasema.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Paschal Mkumbo anaeleza kuwa japokuwa hapingi suala la utengenezaji wa barakoa hizo ila anashauri pawepo na wataalam wa afya wanaokagua kabla ya kutumika.
Mkumbo anasema mazingira hayakuwa masafi ya barakao hizo za vitambaa kwani alikuwa anashuhudia watu wanavyonunua kwa mafundi wa nguo na kuzivaa muda huo huo mdomoni bila kufua au kuzipasi.
Anasema jamii inapaswa kupatiwa elimu kuwa barakoa ambazo zinaninginizwa tuu bila kuwekwa kwenye mazingira ya kufunikwa zinapaswa kufanyiwa usafi kwanza kabla ya kutumika ili kuepuka magonjwa mengine ambayo hayahusiki na UVIKO-19.
Anaongeza kuwa watu wanaweza kupata magonjwa mengine ya kifua ikiwemo pumu kwa kutumia barakoa chafu bila kuzifanyia usafi hivyo kuepuka UVIKO-19 na kupata maradhi mengine kutokana na kutofanyiwa usafi kabla.
“Mimi siyo mtaalam wa afya, ni sawa barakoa inapaswa kuvaliwa ili kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 ila wakaguzi wangepaswa kukagua kwanza na siyo kila mwenye utaalam wa kushona nguo anatengeneza tuu barakoa yake na watu wananunua na kuvaa bila kufua na kuipiga pasi,” anamalizia Mkumbo.