Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamati ya amani Mkoa wa Mwanza ambayo inayoundwa na viongozi wa dini mbalimbali imewataka viongozi wa dini kuwaelimisha waumimini wao umuhimu wa kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agositi 23 mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa leo Juni 28,2022 kwenye mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini mbalimbali, kamati ya amani Mkoa wa Mwanza pamoja na viongozi wa kamati ya amani za Wilaya zote zilizopo Mkoani hapa.
Akizungumza kwenye mkutano huo shekhe wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke ambae pia ni Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani Mkoa wa Mwanza,amesema wameamua kutoa elimu kwa viongozi wa dini kutokana na kwamba viongozi hao wana idadi kubwa ya waumimini hivyo wanaamini elimu hiyo itawafikia vizuri Wananchi na watashiriki kikamilifu katika kukamilisha zoezi hilo.
Aidha,amewataka viongozi wa dini kuendelea kusaidia katika suala zima la malezi ya kiroho ili kuweza kujenga Jamii yenye kumcha Mungu.
Kwa upande wake Charles Sekelwa ambae pia ni Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani Mkoa wa Mwanza,amesema kuwa ni vizuri sana kuieleza Jamii juu ya suala la sensa ili waweze kuelewa na kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.
Mchungaji Esther Raymond kutoka Kanisa la Tabernacle gospel church lililopo kata ya Butimba Mkoani Mwanza,amesema elimu aliyoipata itamsaidia kuwaelimisha waumini wake umuhimu wa sensa ili zoezi la kuhesabiwa litakapoanza jamii iwe na uelewa.
Naye, Halima Jarufu ambae ni mjumbe wa kamati ya amani ya viongozi wa dini Mkoani Mwanza,amesema amepata elimu ambayo itamsaidia kuielimisha jamii umuhimu wa kuhesabiwa huku akiwaasa wanawake kuachana na maneno ya mitani ambayo yanasema sensa haina umuhimu.
Awali akifungua Mkutano huo Katibu tawala Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike,amesema kila mwananchi anatakiwa kuhesabiwa ili kuweza kuisaidia Serikali kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi.