Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akizindua huduma ya ‘Go na NMB’ visiwani Zanzibar. Wakishuhudia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna (wa tatu kutoka kulia), Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi, Filbert Mponzi (wa pili kutoka kulia) Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Shaame na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja – Rashid Simai Msaraka.
………………………………………..
Benki ya NMB imelizindua rasmi jukwaa la kuwawezesha vijana la “GO na NMB” Visiwani Zanzibar na kusema iko tayari kusaidia kuwajenga kiuchumi na kuwakwamua kifedha kwa kuwahudumia kidigitali, kuwakopesha na kuwapa elimu ya fedha.
Akiuelezea mpango huo wenye manufaa lukuki mbele ya mgeni rasmi aliekuwa Makamu wa Pili wa Rais, Ndugu – Hemed Suleiman Abdulla, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Bi Ruth Zaipuna, alisema benki hiyo iko vizuri kiteknolojia kusaidia kuyabadilisha maisha ya vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Bi. Ruth alisema jukwaa la Go na NMB limekuja na fursa mbalimbali kwa vijana ikiwemo; Mikopo ya vitendea kazi mfano mkopo wa pikipiki (Mastaboda), boti (Mastaboat) na mingine mingi. elimu ya kifedha na ujasiriamali, bima mbalimbali ikiwemo bima ya simu bila malipo ya ziada, fursa za ajira kupitia programu ya uongozi kwa wanafunzi waliohitimu chuo (Management Trainee)
Lakini pia, kuwapa elimu kuhusu huduma za kidigitali kama NMB Lipa Mkononi, NMB Mshiko Fasta na NMB Pesa Wakala ambayo mbali ya matumizi ya kuweka na kutuma fedha, inaleta ajira kwa vijana na wengine kutimiza ndoto zao.
Kupitia masuluhisho ya jukwaa hili, Benki ya NMB imejipanga kuwafikia vijana wote wa zanzibar, kuanzia wanafunzi mpaka vijana wenye shuguli za uzalishaji kwenye sekta zote za uchumi na litawahamasisha vijana kujiwekea akiba na kuweka mikakati ya kuwa na shughuli za uzalishaji na kuwahakikishia vipato wakati wote
Katika hotuba yake, Makamu wa Pili wa Rais, Ndugu – Hemed Suleiman Abdulla alisema, jukwaa hili linaendana na juhudi za Serikali za kutatua changamoto zinazowakabili vijana visiwani humo, na limekuja wakati muafaka, kwani ni uwekezaji wenye tija kwa sababu kuwainua vijana kifedha na kiuchumi kutasaidia sana kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Aidha, aliwapongeza NMB kwa hatua hii waliyofikia katika kuhakikisha wanawakwamua vijana pale walipo na kuwatengeneza uwezo wa kuwa na nidhamu ya fedha.