Na Mwandishi wetu, Babati
MKUU wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Lazaro Twange amewakabidhi pikipiki saba maofisa ushirika wa Halmashauri zote za mkoa wa Manyara ili ziweze kuwasaidia kuwafikia wana ushirika na kutoa huduma zenye tija.
Twange amekabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ambaye alitakiwa kuwa mgeni rasmi kwenye jukwaa la tatu la maendeleo ya ushirika.
Amesema pikipiki hizo zikitumika vizuri zitasaidia kuongeza uzalishaji wa wanachama wa vyama vya kilimo na masoko (AMCO’S).
“Kilimo ndiyo sekta pekee ambayo inaweza kuajiri watu wengi kwa wakati mmoja na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” amesema Twange.
Ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa vitendea kazi hivyo ambavyo vitakuwa mkombozi vikitumiwa vizuri na maofisa ushirika.
Mrajis msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Manyara Venance Msafiri amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa pikipiki hizo ambazo zimeondoa tatizo la ukosefu wa usafiri kwa maofisa ushirika.
Msafiri amevitaja vikwazo wanavyokabiliana navyo ni baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri kushindwa kuwasilisha makato ya fedha za watumishi ambao wako kwenye vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na migogoro ya mashamba.
“Pia maofisa ushirika kuendelea kuwa kwenye mamlaka mbili na kazi za ushirika kukwama baada ya kuwa wanapangiwa majukumu mengine hivyo kushindwa kuwajibika ipasavyo,” amesema Msafiri.