Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH ) Dkt.Amos Nungu (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 27,2022 katika Ofisi za Tume hiyo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mratibu wa Mabaraza ya Sayansi Kusini mwa Jangwa la Sahara Bi.Neema TindamanyireMkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH ) Dkt.Amos Nungu akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 27,2022 katika Ofisi za Tume hiyo Jijini Dar es Salaam.Mratibu wa Mabaraza ya Sayansi Kusini mwa Jangwa la Sahara Bi.Neema Tindamanyire akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 27,2022 katika Ofisi za Tume hiyo Jijini Dar es Salaam.
*****************************
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH ) Dkt.Amos Nungu amewataka watafiti kujitokeza na kuandika maandiko ambayo yatawawezesha kupata takribani shilingi Bilioni 20 katika maeneo yanayogusa jamii yakiwemo ya ustawi wa binadamu, mazingira na uchumi endelevu.
Ameyasema hayo leo Juni 27,2022 Dkt.Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za tume hiyo Jijini Dar es Salaam kuhusu fedha hizo zinazotolewa na Mabaraza ya Utafiti Duniani.
Aidha Dkt.Nungu amesema ili kupata fedha hizo inawabidi watafiti mbalimbali nchini kujitokeza na kuandika maandiko ambayo yatashindanishwa na mengine katika maeneo yaliyotajwa yakiwemo ya mifumo ya chakula, mifumo lishe, nishati na maendeleo ya mijini.
“Hii fursa imefunguliwa toka Mei 15, mwaka huu inaenda mpaka Agosti 28 mwaka huu ndipo dirisha linafungwa kwa ile ya kuandika andiko la awali,” Amesema Dkt.Nungu.
Amesema Costech ni miongoni mwa mabaraza ya utafiti 11 duniani ambayo wameweka fedha pamoja kwa ajili ya utafiti chini ya mwavuli wa ‘Global Research Counsel’ ambao ni mwavuli wa mabaraza yote ya utafiti duniani.
Pamoja na hayo amesema kati ya nchi hizo 11, Afrika zipo Tanzania, Kenya na Côte d’Ivoire, pia kuna nchi kutoka mabara ya Ulaya, Asia na Amerika Kusini.
Nchi nyingine ni Chile, China, Afrika Kusini, Switzerland, Sweden, Tanzania, Uturuki, Côte d’Ivoire , Kenya, Netherland na Norway.
“Hizi nchi wameweka fedha pamoja kwa makubaliano kwamba kila nchi inafadhili watafiti kutoka nchini kwake waunde timu ya pamoja iwe na takribani nchi tatu hizo nchi tatu lazima moja itoke Kusini nyingine Kaskazini,” Ameeleza
Ameeleza kuwa kikubwa kinachotakiwa katika kuomba ufadhili huo ni umahiri wa kuandika mradi, watafiti watakaofanikiwa nafasi hiyo Costech itaongea na serikali kuongeza fedha kwa sababu kwa watakaoshinda tume hiyo imetenga sh million 120 kwa kila mradi.