Balozi wa Tanzania Nchini Korea,Mhe.Balozi Togolani Edriss Mavura akimkabidhi zawad Mwenyekiti wa Maandalizi ya maonesho ya Seoul International Travel Fair, Shin, Joong-mok
********************
Tanzania imefanikiwa kupata Tuzo la kuwa na banda bora lenye ubunifu wa kutangaza utalii katika maonesho ya 37 ya utalii ya Seoul International Travel Fair (SITF). Maonesho hayo yaliyofanyika katika jiji la Seoul nchini Korea Kusini kuanzia tarehe 23 – 26 Juni 2022.
“Tuzo hii ni ishara nzuri ya ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau wa Utalii wa Tanzania katika kuandaa ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya SITF. Tutaendelea kuzijongea fursa za kutangaza utalii wa Tanzania na kushiriki katika matukio mbalimbali yatayofanyika hapa Korea”.
Hayo ameyasema Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mhe. Balozi Togolani Edriss Mavura wakati anakabidhiwa Tuzo hiyo na Mwenyekiti wa Maandalizi ya maonesho ya SITF, Mhe. Shin, Joong-mok. Makabidhiano hayo yalifanyika katika Banda la Tanzania.
Banda la Tanzania lilipambwa kwa kuonyesha vivitio mbalimbali vinavyopatikana nchini Tanzania ambapo picha za Utalii wa kutamaduni, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Zanzibar, nyumbu wanaovuka Mto Mara, na madini ya Tanzanite zimewavutia wageni wengi waliotembelea maonesho hayo.
Katika Banda la Tanzania wananchi wa Korea waliweza kujitokeza kwa wingi kunywa na kufurahia radha ya kahawa ya Tanzania , Tukio hili lilichangia Banda la Tanzania kutembelewa na wageni wengi.. Kahawa iliyotumika kwenye maonesho haya ni ile inayolimwa katika wilaya ya mbinga mkoani Ruvuma.
Aidha, Wanawake wengi wa waliotembelea banda la Tanzania walivutiwa sana na usisi wa nywele ambapo walijitokeza kwa wingi kusuka nywele zao. Jambo ambalo walionyesha kulifurahia sana.
Kwa upande wa Bodi ya Utalii Tanzania, Afisa Habari na Uhusiano, Bi, Augustina Makoye amesema “Tunaendelea kubuni njia mbalimbali za kutangaza utalii wa Tanzania ili vivutio vya Tanzania viweze kujulikana zaidi katika soko hili ambalo wananchi wengi wameonyesha kuvutiwa zaidi na vitu vya kiutamaduni, tutaendelea kuliwekea mkakati wa kutangaza utalii wa kiutamaduni kwa vitendo ili tuweze kuwavitia watalii wengi wa nchi ya Korea Kusini.