Na Mwandishi wetu, Babati
VYAMA vya ushirika Mkoani Manyara, vimepatiwa elimu endelevu mjini Babati kwenye ukumbi wa River Nile katika jukwaa la ushirika.
Mrajis msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Manyara, Venance Msafiri amesema lengo la kufanyika kwa jukwaa hilo ni kutoa elimu na kubadilishana uzoefu kwa wana ushirika wa wilaya tano za Manyara.
Msafiri amesema wana vyama 15 ambavyo ni Saccos na vingine vinafanyiwa kazi kwa utaratibu wa kukamilisha usajili ili kukidhi vigezo vya kufanya kazi yao.
“Hadi hivi sasa mkoa wa Manyara una vyama vya ushirika 23 ambavyo vina leseni japokuwa mkoa una jumla ya vyama hai 65,” amesema Msafiri.
Mrajis msaidizi wa huduma za kifedha wa tume ya maendeleo ya ushirika, Josephat Kisamalala aliyemwakilisha Mrajis na mtendaji mkuu wa tume, amesema vyama vya ushirika ambavyo havijapata usajili na vinajihusisha na ukusanyaji fedha vitachukuliwa hatua kali baada ya Serikali kutunga sheria.
Kisamalala amesema ni jinai kwa vyama vya ushirika ambavyo havijasajiliwa, kuendesha shughuli za ukusanyaji fedha ili hali havijakata leseni.
Amesema zaidi ya Saccos 1,000 zinatakiwa kufutwa na vyama vya ushirika wa kilimo na masoko (Amcos) zaidi ya 3,000 havijaomba kupata leseni ili kuendana na sheria ndogo ya huduma za kifedha ya mwaka 2018.
Kisamalala amesema tangu kuanza kutumika kwa sheria ndogo ya huduma ya fedha mwaka 2018 maombi ya leseni 1,155 yalitolewa.
“Kati ya maombi 1,155 yaliyopokelewa, walitoa leseni kwa vyama vya akiba 692 na kukataa maombi ya vyama 463 nchini,” amesema Kisamalala.
Mwenyekiti wa jukwaa la ushirika mkoani Manyara, Lohay Langai amesema sheria hiyo ni nzuri na itasaidia kuondoa kufanya biashara holela kama awali.
“Sheria hiyo itawafungua macho na itazidi kufufua vyama vya ushirika vilivyolala na kuwa macho vikifanya kazi,” amesema Langai.