Balozi Togolani Edriss Mavura akiongea na Wadau wa Utalii wa nchi ya Korea kusini.
Afisa Habari na Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania, Augustina Makoye akiongea wakati wa kutoa neno la shukrani kwa wadau wa Utalii waliohudhuria mkutano na wadau wa utalii wa Korea kusini.
Mhe. Balozi Togolani Edriss Mavura akijadili jambo na Afisa Habari wa Bodi ya Utalii Tanzania, Augustina Makoye wakati wa mkutano na wadau wa utalii.
Picha ya pamoja ya Mhe. Balozi Togolani Edriss Mavura na Mawakala na Waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo.
………………………………………………
Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini imetumia maonesho ya Seoul International Tourism Expo (KOTFA 2022), kuonesha Makala ya The Royal Tour Tanzania kwa Mawakala wa utalii pamoja na Waandishi wa habari za utalii katika soko ya utalii nchi hiyo. Maonesho yameanza tarehe 23 – 26, 2022.
“Nashukuru leo tumefanikiwa kukutana na wadau wa utalii wa hapa Korea Kusini, huu ni mwanzo mzuri na tutaendelea na utaratibu huu ili wadau waweze kuvijua zaidi vivutio vya utalii vya Tanzania. Baada ya kuona filamu ya The Royal Tour, TANZANIA, wamependa kujua fursa za uwekezaji zilizopo Tanzani, jambo ambalo linaleta matumaini kwa Mawakala wa utalii wa nchi hii kuanza kuuza utalii wa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Edriss Mavura wakati wa mkutano uliofanyika Juni 24, 2022 katika hotel ya Intercontinental Seoul Pama iliyopo katika mji wa Seoul.
Naye Afisa Habari na Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bi. Augustina Makoye ametumia mkutano huo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Korea Kusini kwani Tanzania bado ina fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii hasa kwa upande wa Malazi, Migahawa na huduma nyingine, ili iwe chachu ya kuwavutia watalii wengi kutoka katika soko la utalii la Korea.
Aidha, wakati anatoa neno la shukrani, Bi. Augustina ametumia muda huo kuwaalika Mawakala wa utalii wa Korea Kusini kushiriki Onesho la Utalii la Swahili International Tourism Expo (SITE) linaloandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania. Onesho hilo limepangwa kufanyika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam, na ameahidi kuwatumia mwaliko punde maandalizi ya onesho hilo yatakapo zinduliwa rasmi.