Na Dotto Mwaibale, Singida
WANAFUNZI wa shule zote za msingi za Serikali na zisizo za Serikali katika Mkoa wa Singida, watagawiwa vyandarua kuanzia Julai mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa afua zakupambana na
ugonjwa wa malaria nchini.
Mratibu wa Malaria Mkoa wa Singida, Dk.Abdallah Balla, alisema hayo
wakati akizungumza na waandishi wa
habari mjini hapa na kwamba vyandarua hivyo vitagawiwa kwa wanafunzi wa kuanzia
darasa la kwanza hadi saba.
Dk.Balla alisema zoezi la kugawa vyandarua hivyo ambavyo vitakuwa takribani
200,000 litaanza mara baada ya Bohari ya Dawa (MSD) kuvitoa na kuanza
kuvipeleka mashuleni.
Dk.Balla alisema vyandarua hivyo vitagawiwa bila kujali wapo wangapi kwenye
kaya kwani lengo la serikali ni kutaka kuifanya Tanzania iwe huru kwa ugonjwa
wa malaria ifikapo 2030.
Aliongeza katika kuhakikisha zoezi la kugawa vyandarua hivyo linafanikiwa,
viongozi wa dini wamepewa semina ili wasaidie kuwaelimisha wananchi kwenye
nyumba za ibada umuhimu wa vyandarua
hivyo.
Aliwataka wananchi waendelee kutunza mazingira kwa kuondoa maeneo ambayo
maji yanaweza kutuwama kwani ndiyo yanakuwa chanzo cha mazalia ya mbu.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Waadiventisti Wasabato Wilaya ya Manyoni, Joel Ndegea,
alisema wananchi watambue kuwa serikali imetumia fedha nyingi kununua vyandarua
hivyo wahakikishe wanavitumia kupambana na malaria na sio kwenda kuvitumia
kuvulia samaki au kufugia kuku.
Kwa upande wake Mratibu wa Kamati ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Singida, Happy
Francis, alisema vyandarua hivyo vimekuja katika muda mwafaka hivyo wanafunzi
watakapogawiwa wazazi wahakikishe wanavitumia kwa malengo yanayosudiwa na si
vinginevyo.
Mwenyekiti wa Kamati za Dini Mkoa wa Singida, Khamis Kisuke, aliipongeza
serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kutoa vyandarua hivyo
na kuahidi kuwa watahakikisha wanawahamasisha wananchi ili wavitumie kwa lengo
la kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.