Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki chini ya uongozi wa Waziri
Liberata Mulamula imeendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza nchi na
fursa zake kama sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. Katika
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaohitimishwa leo
tarehe 25 Juni 2022 nchini Rwanda na kuhudhuriwa takribani na viongozi wa
kaliba na ngazi tofauti wa nchi zote 54 za umoja huo, Tanzania ilitumia fursa
hiyo kuhamasisha wawekezaji na kuja nchini. Balozi
Liberata Mulamula alionekana akifanya mazungumzo rasmi na yasiyo rasmi na
Mawaziri wenzake wa Mambo ya Nje na hata Mawaziri Wakuu na Marais wa nchini
mbalimbali kwa lengo la kuitangaza nchi. Alisikika akiwaambia, “Rais wetu, Mhe.
Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kuboresha
mazingira ya biashara, hivyo milango ipo wazi, waambieni wafanyabiashara wenu
waje kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali na hasa kilimo ambacho ni moja
ya kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita”. Viongozi
ambao Mhe. Waziri Mulamula alipata fursa ya kufanya nao mazungumzo rasmi ni
pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan;
Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe.
Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina
Rabbani Khar na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa
Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair. Viongozi
Wakuu aliokutana nao na kuwapa salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa
Canada, Mhe. Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Zambia,
Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta; na Rais wa
Nigeria, Mhe. Muhammadu Buhari. Katika
mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula alihimiza ushirikiano
katika biashara na uwekezaji, mafunzo, usafiri wa anga na utalii. Alieleza namna Serikali ya awamu ya sita
inavyofanya jitihada kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuboresha mazingira ya
uwekezaji ili kushawishi wawekezaji wengi. Aliziomba Canada, Singapore, India
na Pakistan kuleta wawekezaji wengi zaidi na hasa katika sekta ya kilimo ambayo
ni kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita. Kuhusu
utalii, Mhe. Waziri aliziomba nchi hizo kutafsiri Filamu ya The Royal Tour
iliyoongozwa na Rais Samia kwa lugha za nchi zao ili iwafikie watu wengi zaidi.
Aidha, alizihimiza nchi hizo, hususan India na Singapore kuanzisha safari za
moja kwa moja za mashirika yao ya ndege kati ya Tanzania na nchi hizo ili
kuhamasisha utalii. Aidha,
Mhe. Waziri alihimiza ushirikiano na Singapore katika Uchumi wa Buluu kutokana
na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kwenye eneo hilo, hususan kwenye uendelezaji,
usimamizi na uendeshaji wa bandari. Aligusia pia umuhimu wa kujengeana uwezo
hususan katika eneo la rasilimali watu na mafunzo ya TEHAMA. Wakati
wa mazungumzo na Bibi Cherie Blair, alielezea utayari wa Mfuko wake wa Cherie
Blair Foundation wa kushirikiana na Tanzania, kwenye kuwajengea uwezo
wanasheria wa kuwa na ujuzi wa kutosha wa upatanishi na usuluhishi wa migogoro
nje ya mahakama na kwamba mfuko huo pia, upo tayari kuisaidia Tanzania kwa
kutoa msaada kwa mawakili katika kesi za Kimataifa zinazoikabili Serikali ya Tanzania. Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola utafungwa leo jioni na Balozi
Mulamula ataendeelea na mkakati wake wa kukutana na viongozi mbalimbali na
atarejea nchini tarehe 26 Juni 2022.
|