Kaimu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST),Prof. Antony Mshandete akiongea na washiriki wa Warsha ya kuwajengea uwezo Washauri wa Wanafunzi na Viongozi wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu wakati wa kufunga Warsha hiyo Juni 24, 2022 Jijini Arusha.
Kaimu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela(NM-AIST), Prof. Antony Mshandete(kulia) akitoa vyeti kwa washiriki wa Warsha ya kuwajengea uwezo Washauri wa Wanafunzi na Viongozi wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu wakati wa kufunga Warsha hiyo Juni 24, 2022 Jijini Arusha.
………………………………………
Na. Mwandishi Wetu
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Afrika Sayansi na Teknoloji ya Nelson Mandela Prof. Antony Mshandete ametoa wito kwa Chama cha Washauri wa Wanafunzi Tanzania (TACOGA1984) kuja na mkakati wa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu.
Prof. Mshandete alisema hayo Juni 24, 2022 wakati wa kufunga warsha ya siku tatu ya Washauri wa Wanafunzi na Viongozi wa Serikali za Wanafunzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu yaliyoandaliwa na TACOGA1984 jijini Arusha.
“Wito wangu kwa TACOGA1984, mje na mkakati wa jinsi ya kukabiliana na mmonyoko wa maadili na kuuwasilisha kwa kamati ya Wakuu wa vyuo ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya juu” alisema Prof. Mshandete
Aliongeza kuwa, vyuo vya elimu ya juu vya umma na binafsi vinakabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili ikiwemo mavazi ,lugha na unyanyasi wa kijinsia hivyo TACOGA1984 kuwa mstari wa mbele katika kushauri na kuwaongoza wanafunzi ili kujenga jamii bora.
“Ninyi ni nguzo muhimu katika kusimamia maono ,dhamira na maadili ya msingi ili malengo ya TACOGA1984 yaweze kuzaa matunda yatakayodumu” alisisitza Prof. Mshandete
Naye Mwenyekiti wa TACOGA1984 Bibi.Sophia Nchimbi, amewataka washiriki wa warsha hiyo kufanyia kazi yale yote waliyojifunza ili kuleta matokeo chanya katika utendaji wao kwa kuwashauri na kuwaongoza vyema wanafunzi ili kujenga jamii yenye maadili mema.
“Naamini mtaenda kutekeleza kwa vitendo haya yote mliyojifunza ,sisi kama kamati tendaji tutafanya ufuatiliaji wa karibu kujua kama haya mafunzo yamefanyiwa kazi “alisema Bibi.Sophia Nchimbi
Aidha, Bi Sophia aliwataka wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo kuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwa wanafunzi wenzao na jamii zinazowazunguka .
Warsha ya kuwajengea uwezo Washauri wa Wanafunzi na Viongozi wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu ilianza Juni 21, 2022 na kumalizika Juni 24, 2022 kwa kuangazia mada zipatazo 16 ikiwemo jinsi ya kujihusisha na ushauri wa kitaalamu, mbinu za uendeshaji masuala yahusuyo nidhamu kwa wanafunzi wa elimu ya juu na urejeshaji wa mahusiano mema kati ya wanafunzi.